Russia: Marekani inapasa kufuta vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa huko Vienna Austria amesema kwamba Marekani inapasa kuondoa mara moja vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakati huohuo kuchukua hatua za kufidia makosa na ukiukaji wake dhidi ya mapatano ya kimataifa ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumzia suala hilo hapo jana Jumatano, Mikhail Ulyanov aliashiria hatua ya Iran ya kusimamisha kwa muda uwajibikaji wake kuhusiana na baadhi ya vipengee vya mapatano hayo na kusema kuwa Marekani ilijotoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo muhimu ya nyuklia na kuanza kutekeleza vikwazo vya ndani na visivyo vya kisheria dhidi ya Iran ili kuwashawishi wanachama wengine wa mapatano hayo wafuate mfano wake huo lakini ikawa imefeli vibaya.
Mikhail Ulyanov ameongeza kuwa msimamo wa Iran unabainisha wazi kuwa imeazimia kulinda mapatano ya JCPOA kwa sharti kwamba pande nyingine za mapatano hayo nazo ziwe tayari kutekeleza majukumu na ahadi zao za kuidhaminia Tehran maslahi yake ya kibiashara na kiuchumi. Marekani inapasa kuheshimu ahadi zake na kufidia mara moja ukiukaji wake na vilevile kuondoa vikwazo vya upande mmoja ilivyoiwekea Iran baada ya kujiondoa katika mapatano hayo mwaka 2018.
Ulyanov pia amezitaka nchi nyingine zilizosalia katika mapatano hayo zitekeleze ahadi zao kwa Iran. Rais Donald Trump wa Marekani aliitoa nchi hiyo katika mapatano ya JCPOA tarehe 8 Mei 2018.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ilitangaza tarehe 8 Mei mwaka uliofuata wa 2019, kwamba ingeanza kupunguza baadhi ya uwajibikaji wake katika mapatano hayo na kwa msingi wa vipengee vya matano hayo hayo, baada ya kuthibitika wazi kuwa nchi za Ulaya zilikuwa zimeshindwa kuifidia Iran hasara ya kiuchumi iliyosababishwa na hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani.