Trump: Uchaguzi wa Marekani ulikuwa ni uvurundo mtupu
Rais wa Marekani amesema kuwa, uchaguzi wa Novemba 3, 2020 nchini humo ulikuwa uvundo na uvurundo mtupu.
Donal Trump amesema hayo katika sherehe maalumu zilizofanyika katika Ikulu ya Marekani, White House na kuongeza kuwa, matokeo ya uchaguzi wa rais wa Novemba 3 wa nchi hiyo yamechakachuliwa na uvurundo wote uliokuwemo kwenye uchaguzi huo umefanyika kwa madhara yake.
Rais huyo wa Marekani kama kawaida yake, kwa mara nyingine ameonesha dharau zake kwa mataifa mengine akisema, uchaguzi huo wa Marekani haukuwa na tofauti yoyote ya chaguzi zinazofanyika katika nchi za ulimwengu wa tatu.
Vile vile amedai kwamba yeye ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo.
Matamshi hayo ya Trump yamekuja licha ya msemaji wa White House, Kayleigh McEnany kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba Donald Trump hakushinda katika uchaguzi huo. McEnany amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mahojiano maalumu kwamba Joe Biden ndiye mshindi wa uchaguzi wa Novemba 3, 2020 huko Marekani.
Majumuisho ya vyombo vya habari vya Marekani yanaonesha kuwa Donald Trump amebwagwa vibaya katika uchaguzi huo na kwamba Joe Biden amefanikiwa kupata kura 306 mbele ya kura 232 za Electoral College za Donald Trump.
Timu ya uchaguzi ya Trump hadi hivi sasa imekataa kukubali kushindwa na imefungua mashtaka katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo kulalamikia uchakachuaji mkubwa wa kura. Hata hivyo mashtaka yao yamekataliwa.