Kukamatwa watu 150 katika maandamano ya Paris
(last modified Sun, 13 Dec 2020 09:06:54 GMT )
Dec 13, 2020 09:06 UTC
  • Kukamatwa watu 150 katika maandamano ya Paris

Mji wa Paris nchini Ufaransa umeshuhudia ghasia na maandamano mapya ya kupinga muswada wa usalama uliowasilishwa bungeni na serikali ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo, ambapo watu 150 wametiwa nguvuni katika maandamano hayo.

Kanali ya Russia Today imeripoti kwamba maelfu ya Wafaransa wamemiminika mitaani mjini humo kwa wiki ya tano mfululizo, ikiwa ni katika maandamano yanayofanyika mwishoni mwa wiki kupinga marekebisho kuhusu masuala ya usalama yaliyowasilishwa bungeni na serikali ya Macron.

Picha za video zilizochukuliwa katika maandamano hayo ya Paris zimeonyesha waandamanaji waliokuwa na hasira kubwa wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa maneno na nara zinazosema, 'zuieni sheria zinazoua uhuru' na 'zuieni chuki dhidi ya Uislamu.'

Kufuatia kuongezeka maandamano dhidi ya serikali huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa, serikali ya Macron imekuwa ikitumia nguvu za ziada kuvunja maandamano hayo.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimesema kuwa kufikia jana jioni idadi ya waandamanaji waliokuwa wametiwa nguvuni na polisi katika maandamano hayo ilikuwa 150.

Ukatili wa polisi ya Ufaransa

Katika siku za karibuni, Ufaransa imekuwa ikishuhudia maandamano na ghasia kubwa zinazotokana na upinzani wa raia wa nchi hiyo dhidi ya muswada wa marekebisho ya usalama uliowasilishwa bungeni na serikali ya Rais Macron, muswada ambao utawezesha askari usalama wa nchi hiyo kupewa vifaa zaidi vya ujasusi dhidi ya raia na wakati huo huo kutohukumiwa mahakamani wanapotumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji.

Mada ya 24 ya muswada huo inapiga marufuku kuchukuliwa picha za maafisa wa polisi wanapokuwa wanawakandamiza waandamanaji na watuhumiwa kupewa kifungo cha mwaka mmoja au kutozwa faini ya Euro elfu 45 wanapopatikana na hatia.

Kufuatia kuongezeka maandamano ya kupinga muswada huo, viongozi wa Ufaransa wamelegeza msimamo na kuahidi kuufanyia marekebisho kabla ya kuurejesha tena bungeni.