Chombo cha China kilichofika mwezini charejea duniani
Chombo cha anga za mbali cha China kinachojulikana kama Chang’e -5 kilichorushwa kwenda kwenye mwezi, mapema leo kimetua duniani kikiwa na sampuli za kwanza zilizokusanywa kutoka kwenye mwezi, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha 40.
Idara ya Taifa ya Mambo ya Anga za Mbali ya China imesema chombo hicho kimetua usiku wa manane katika mkoa wa Mongolia ndani ya China.
Mkuu wa Idara hiyo Bw. Zhang Kejian amesema mpango mzima wa safari ya chombo hicho umefanikiwa.
Chombo hicho kitasafirishwa hadi mji mkuu, Beijing, na sampuli zake zitafanyiwa uchunguzi na jopo maalumu la watafiti.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Mwezi katika Idara ya Taifa ya Mambo ya Anga za Mbali ya China Bw. Pei Zhaoyu, amesema China itatoa baadhi ya sampuli hizo kwa wanasayansi wa nchi nyingine.
Mpango mzima wa chombo hicho kilichorushwa kwenda kwenye mwezi tarehe 24 Novemba, ulikuwa na changamoto nyingi katika historia ya utafiti wa anga ya mbali ya China.