Iran yasisitiza nchi za Ulaya zitumie mfumo wa INSTEX
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kuthibitisha kuwa mfumo wa mabadilishano ya kifedha na Iran maarufu kama Instex unafanya kazi ili Iran iweze kunufaika kiuchumi na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Majid Takht-Ravanchi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika tathmini ya Iran kuhusu ripoti ya 10 ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu azimio 2231. Takht Ravanchi amebainisha mtazamo huo wa Iran katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi Jerry Matjila wa Afrika Kusini.
Azimio nambari 2231 lilipasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA mwaka 2015 na kila miezi sita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatakiwa kuwasilisha ripoti kwa Baraza la Usalama kuhusu utekelezwaji wa azimio hilo.
Katika barua yake, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani ni mkiukaji mkubwa wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Amesema hatua ya Iran kupunguza majkumu yake katika JCPOA imetokana na ukiukaji wa mapatano hayo uliotekelezwa na upande wa pili. Aidha amesema hatua ambazo Iran imezichukua ni kwa mujibu wa haki zake zilizoanishwa katika mapatano hayo ya JCPOA.
Akiashiria ahadi ya nchi za Ulaya kuhakikisha kuwa uhusiano wa kiuchumi na Iran utaendelea kama ilivyotabiriwa katika mapatano ya JCPOA sambamba na kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya kifedha wa Instex, Takht-Ravanchi amesema mfumo huu sasa unapaswa kuthibitisha ubora wake baada ya miaka miwili kupita.

Akiashiria mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran Shahidi Mohsen Fakhrizadeh, amesema namna mauaji hayo yalivyoashiriwa katika ripoti hiyo ya 10 haitoshi.
Ameongeza kuwa, mauaji ya Shahidi Fakhrizadeh mwezi uliopita wa Novemba na mauaji ya Januari mwaka huu ya Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani ni vitendo vya kigaidi na vinapaswa kulaaniwa vikali na wazi wazi.
Mnamo Januari 3 mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump lilitenda jinai kwa kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akiwa uraiani nchini Iraq tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Baghdad.
Naye Dk Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran ambaye pia alikuwa msomi bingwa wa nyuklia aliuawa shahidi jioni ya siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba katika shambulio la kigaidi lililotokea kwenye viunga vya Tehran.