Marais wa Russia na Ufaransa wataka kulindwa mapatano ya JCPOA
(last modified Wed, 23 Dec 2020 12:25:41 GMT )
Dec 23, 2020 12:25 UTC
  • Marais wa Russia na Ufaransa wataka kulindwa mapatano ya JCPOA

Marais Vladimir Putin wa Russia na Emmanuel Macron wa Ufaransa wametoa mwito wa kuweko jitihada za pamoja za kuyalinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin), marais hao wawili walitoa mwito huo jana Jumanne katika mazungumzo yao ya simu.

Taarifa ya idara hiyo ya Kremlin imesema: Kuhusu hali inayouzunguka mradi wa nyuklia wa Iran, pande mbili zimesisitizia haja ya kuwepo ushirikiano wa pamoja wa nchi washirika wa JCPOA ili kuhakikisha kuwa mapatano hayo yanalindwa.

Mwito huo wa Marais Vladimir Putin wa Russia na Emmanuel Macron wa Ufaransa umekuja siku mbili baada ya kufanyika kikao kisicho rasmi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na nchi zinazounda kundi la 4+1 kwa kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Barrell.

Kikao cha nchi wanachama wa mapatano ya JCPOA

Washiriki wa kikao hicho cha Jumatatu walisisitiza juu ya kufungamana na suala la kuyalinda mapatano ya JCPOA na kueleza kuwa: azimio nambari 2231 linapaswa kuendelea kutekelezwa kikamilifu.  

Kadhalika Mawaziri hao wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4+1 kwa mara nyingine tena walieleza kusikitishwa sana na  hatua ya Marekani ya kujitoa kwenye mapatano hayo.  

Tags