Ilhan Omar: Ubaguzi wa rangi bado unatawala Marekani
Mbunge Muislamu katika Kongresi ya Marekani Ilhan Omar amesema kuwa kutohukumiwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump ni ishara ya kuendelea mgawanyiko wa kisiasa na kijamii na vilevile ubaguzi wa rangi katika nchi hiyo. Ilhan Omar ametahadharisha kuhusu athari mbaya za kutohukumiwa Trump katika vikao vya Baraza la Seneti ya Marekani.
Mbunge huyo wa kike wa Marekani amesema kuwa kutotiwa hatiani Donald Trump katika vikao vya Seneti kumeisababishia hasara Marekani.
Mpango wa kumsaili na kumhukumu rais aliyeondoka madarakani wa Marekani, Donald Trump kwa tuhuma za kuchochea uasi na kushambulia jengo la Kongresi umefeli baada ya kutopata kura za thuluthi mbili za wawakilishi wa Baraza la Seneti.
Wakati huo huo mwakilishi huyo Muislamu wa Kongresi ya Marekani amesema kuwa serikali ya Joe Biden inapaswa kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina kwa sababu ujenzi huo unakiuka sheria za kimataifa. Amesema anaunga mkono mpango wa kushtakiwa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa sababu ya uhalifu unaofanywa na utawalka huo dhidi ya watu wa Palestina.
Hivi karibuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitangaza kuwa inayo haki ya kushughulikia jinai na uhalifu unaofanywa na Israel katika mipaka ya mwaka 1967 ya rdhi za Palestina.
Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanaitambua rasmi mipaka ya mwaka 1967 kuwa ndiyo mipaka ya ardhi ya Palestina na yamepiga marufuku ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa kizayuni katika ardhi zote za eneo hilo zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.