Biden akiri, ubaguzi wa rangi unaendelea kuitafuna jamii ya Marekani
Ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kimbari na ukatili dhidi ya watu weusi daima vimekuwa miongoni mwa sifa kuu za jamii ya Marekani tangu nchi hiyo ilipoasisiwa, na hadi sasa Wamarekani weusi wangali wanasumbuliwa na aina mbalimbali za ubaguzi na ukatili.
Huu ndio ukweli ambao hata Rais mpya wa Marekani, Joe Biden, amelazimika kukiri kwamba bado linatawala jamii ya nchi hiyo. Jumatano iliyopita Biden alisema kuwa, ubaguzi wa rangi unashuhudiwa hata katika hukumu zinazotolewa mahakamani. Alisema: "Hapa nchini kwetu Marekani tumeshuhudia mtu mweusi akihukumiwa adhabu kali zaidi kuliko mzungu aliyehukumiwa kwa kosa hilo hilo. Kwa mfano tu, mzungu anahukumiwa kifungo cha miaka miwili lakini Mmarekani mweusi anahukumiwa kifungo cha miaka saba kwa kosa hilo hilo."
Ubaguzi wa rangi na ukatili dhidi ya watu wenye rangi nyeusi nchini Marekani ambao ulianza sambamba na mfumo wa utumwa uliotawala nchini humo katika karne 17, ungalipo hadi hii leo. Wamarekani weusi ambao wao wenyewe wanawaita Waafrika Wamarekani (African Americans), ndiyo jamii ya pili ya waliowachache nchini humo baada ya Walatino (watu wenye asili ya America ya Latini), na wanaunda karibu asilimia 14 ya jamii ya watu wote wa Marekani. Baada ya kuchaguliwa Barack Hussein Obama kuwa rais wa kwanza mweusi wa Marekani (2009-2017) ilitarajiwa kuwa, hali ya Wamarekani weusi ingeboreka; hata hivyo mambo yalikwenda kinyume, na hali ya watu weusi iliendelea kuwa mbaya zaidi kiuchumi, kijamii na kadhalika.

Japokuwa harakati ya kutetea haki za kiraia ya watu weusi ilizusha wimbi la kupigania haki zao na kufutwa ubaguzi nchini Marekani katika muongo wa 1950, lakini hali halisi ya jamii ya nchi hiyo inaonyesha kwamba, ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa kimbari katika nyanja na sura mbalimbali vingali vinaendelea katika nchi hiyo inayodai kuwa kinara wa kutetea haki za binadamu. Miongoni mwa vielelezo vya ubaguzi huo ni kwamba Wamarekani weusi ndio wanaokamatwa na kutiwa mbaroni zaidi kuliko wazungu waliowengi, na ndio wanaojazana katika jela za Marekani. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 67 ya wafungwa wote wa Marekani ni watu weusi. Hata mfumo wa mahakama za Marekani haukusalimika na ubaguzi huo dhidi ya watu weusi. Hii ndiyo maana Joe Biden akakiri uhakika kwamba, pale mtu mweusi anapokabiliwa na tuhuma za kuiba kwa mara ya kwanza hupewa adhabu kali zaidi ya kifungo ikilinganishwa na mzungu anayekabiliwa na tuhuma hiyo hiyo.
Wakati huo huo ubaguzi wa rangi umekuwa na taathira mbaya katika maisha ya kijamii ya Wamarekani weusi na umepelekea kujitokeza mfumo na mwenendo unaowafanya watu wa tabaka hili wawe wahanga wa ubaguzi katika elimu, afya, uchumi, ajira na kadhalika. Vilevile wakati wa migogoro mikubwa kama huu wa sasa wa maambukizi ya virusi vya corona, watu weusi na Walatino ndio wanaoathirika zaidi kuliko wazungu.

Katika upande mwingine Wamarekani weusi ndio wahanga wakuu wa ukatili wa polisi, na suala hili ndilo chachu ya maandamano na uasi wa kijamii unaojitokeza mara kwa mara katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Mfano wa maandamano hayo ni yale yaliyoibuka nchini humo mwaka jana baada ya polisi mzungu kumuua kwa damu baridi Mmarekai mweusi, George Floyd katika mji wa Minneapolis kwenye jimbo la Minnesota. Chanzo cha ukatili huo ni ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika jamii ya Marekani. Kuhusiana na suala hili rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama anasema: Ubaguzi wa rangi umo katika vinasaba (DNA) vya baadhi ya Wamarekani.

Licha ya malalamiko na maandamano ya mara kwa mara ya kupinga mfumo wa ubaguzi na ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi, lakini hadi sasa hakujachukuliwa hatua ya maana na ya kimsingi ya kukabiliana na tatizo hilo, na vyombo vya juu vya utawala wa nchi hiyo vikiwemo vile vya mahakama vinaendelea kupinga juhudi za aina mbalimbali za kuhakikisha ubaguzi wa rangi unakomeshwa kikamiifu nchini humo.