Feb 27, 2021 02:50 UTC
  •  Michelle Bachelet: Saudia ikomeshe ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza masikitiko yake kutokana na ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya raia wa nchi hiyo.

 Michelle Bachelet ameitaka Saudi Arabia iheshimu uhuru wa kusema na haki za raia za kufanya mijumuiko na mikutano ya hadhara.

Saudi Arabia imekuwa ikishutumiwa na mashirika na jumuiya za kuteta haki za binadamu kuokana na kukandamiza haki za raia hususan wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu, wafuasi wa madhehebu za waliowachache hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Wiki kadhaa zilizopita Saudi Arabia ililazimika kumuachia huru mwanaharakati wa haki za wanawake, Loujain al-Hathloul kutokana na mashinikizo ya jumuiya za kimataifa. 

Al-Hathloul mwenye umri wa miaka 31 alifungwa jela nchini Saudi Arabia tangu mwezi Mei mwaka 2018. Mwanaharakati huyo wa kike alikamatwa na kufungwa jela kwa sababu ya kudai uhuru wa mwanamke kuendesha gari Saudi Arabia. Hata hivyo mwendesha mashtaka wa serikali ya nchi hiyo alimbambikia tuhuma za kusababisha madhara kwa maslahi ya taifa. 

 Loujain alikabiliwa na sulubu na mateso mengi katika jela ya serikali ya Saudia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametangaza kuwa, Loujain al-Hathloul amepewa mateso ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuteswa kwa kutumia nyaya za umeme na kunajisiwa.

Al-Hathloul (kushoto) na mrithi wa ufalme wa Saudia, Bin Salman

Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Magharibi yanaitaja Saudi Arabia kuwa ni "ngome ya udikteta" ambako si tu kwamba hata marekebisho ya mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman hayakuweza kupunguza ukatili na manyanyaso yanayofanyika humo, bali ukandamizaji wa kisiasa na wa mahakama unaendelea kushika kasi zaidi. Hii ni kwa sababu marekebisho hayo ya Bin Salman hayakuwa ya kimsingi, na zaidi ilikuwa hatua ya kimaonyesho.

Tags