Ufaransa: Azimio dhidi ya Iran litapigiwa kura siku zijazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuwa azimio la kuikosoa Iran limepangwa kupigiwa kura siku zijazo katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Jean Yves Le Drian jana usiku alitangaza kuwa, azimio lililopendekezwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani linalokosoa hatua ya Iran ya kupunguza ushirikiano wake kwa wakala wa IAEA litapigiwa kura siku zijazo katika Bodi ya Magavana ya wakala huo.
Azimio hilo linatazamiwa kupigiwa kura katika Bodi ya Magavana huku Iran na Russia zikizitahadharisha vikali pande za Magharibi juu ya taathira hasi za kupasishwa azimio kama hilo. Iran pia imetahadharisha kuwa, kupasishwa azimio kama hilo dhidi yake hakutakuwa na faida yoyote na inaitathmini hatua hiyo kuwa sawa na kufikia mwisho taarifa ya pamoja ya Februari 21 kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Iran na IAEA tarehe 2 mwezi Februari zilikubaliana kuismamisha kikamilifu kwa hiari utekelezaji wa protokali ya ziada; na ushrikiano wake na wakala huo utaendelea kwa mujibu taratibu za kawaida tu za ukaguzi wa shughuli zake za nyuklia. Aidha kwa mujibu wa sheria iliyoidhinishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, Wakala wa IAEA hautaruhusiwa kukagua maeneo zaidi ya Iran na wala ukaguzi wa ziada pia hautafanyika hapa nchini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanzia tarehe 23 mwezi huu imesitisha hatua zake za khiari kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA katika fremu ya sheria ya hatua za kistratejia ili kuondolewa vikwazo na kulinda haki za wananchi wa Iran.