Marekani; tishio kubwa zaidi kwa China
Huku vita vya maneno vikizidi kuongezeka kati ya viongozi wa China na Marekani, mara hii Rais Xi Jinping wa China amesema kuwa Marekani ndilo tishio kubwa zaidi kwa usalama wa nchi yake.
Rais Xi Jinping vile vile ameongeza kuwa Marekani ndilo chimbuko kubwa zaidi la ghasia na fujo duniani. Matamshi ya Jinping yametolewa katika hali ambayo tokea Rais Joe Biden achukue madaraka huko White House, siasa rasmi za Washington zinaendelea kuchukua mkondo wa uhasama dhidi ya Beijing.
Kwa maneno mengine ni kwamba licha ya dhana za awali kwamba siasa za Washington kuhusiana na Beijing zingebadilika na kuchukua sura laini kidogo katika uongozi wa Rais Biden, zikilinganishwa na za mtangulizi wake Donald Trump, lakini matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na maafisa wa serikali yake katika siku za karibuni yanathibitisha wazi kwamba siasa za mabavu za Marekani dhidi ya China hazijabadilika hata kidogo.
Kwa mfano, Jumamosi iliyopita Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliwatumia ujumbe wanajeshi wa nchi hiyo akisema kwamba China ndiyo changamoto kubwa zaidi kwa wizara hiyo na kuongeza kuwa muelekeo wa Marekani kwa China utazingatia maslahi ya kisiasa ya ndani na nje ya Marekani. Bila shaka matamshi kama hayo hayatoki tu kwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani bali yanatolewa na maafisa tofauti wa nchi hiyo akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ambaye awali alinukuliwa akisema kuwa China ndiyo changamoto kubwa ya kwanza inayoikabili Marekani.
Adam Philip Davidson kamanda wa vikasi vya Marekani katika eneo la Bahari ya Hindi na Bahari ya Pacific (USINDOPACOM) hivi majuzi alitaka nguvu ya kijeshi ya Marekani iimarishwe kwa lengo la kukabiliana na China. Akizungumza Jumanne katika kongamano moja, Davidson alisema kwamba tishio kubwa zaidi dhidi ya Marekani ni kupunguzwa nguvu yake ya kawaida ya kijeshi katika eneo la bahari za Hindi na Pacific, kwa hoja kuwa huo ni msingi muhimu katika jeshi hilo.
Swali hili linajitokeza hapa kwamba, je ni kwa nini serikali ya Marekani hujishughulisha kwa nguvu zake zote na siasa za kuongeza uhasama dhidi ya China bila kujali ni serikali ya chama gani inayokuwa madarakani White House? Je, ni lengo gani linalofuatiliwa katika uwanja huo?
Jambo lisilo na shaka yoyote ni kwamba, tofauti za Marekani na China zinatokana na masuala mengi yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kistratijia na kijiopolitiki. Ni wazi kuwa tofauti hizo zimekuwa zikiongezeka katika miaka ya karibuni kutokana na siasa za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, na hasa kuhusiana na Hong Kong, Taiwan na hitilafu za mipaka katika Bahari ya China Kusini na Mashariki.
Ni kutokana na ukweli huo ndipo Rais Xi Jinping akaitaja Marekani hivi karibuni kuwa chanzo cha ghasia na fujo katika dunia ya sasa na vilevile kuitaja kuwa tishio kubwa zaidi kwa usalama na maendeleo ya nchi yake.
Kwa vyo vyote vile mvutano wa China na Marekani unaongezeka katika kipindi hiki cha uongozi wa Joe Biden huko White House katika hali ambayo China imeendelea kulinda kwa mwaka wa 11 mfululizo nafasi yake ya nchi iliyo na ustawi na uzalishaji mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani.
Kwa mujibu wa ripoti ya karibuni ya Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China uchumi wa nchi hiyo unaunda karibu asilimia 30 ya uzalishaji wote wa dunia. Katika miaka mitano iliyopita, kiwango cha wastani cha ustawi wa thamani ya nyongeza uliotokana na uzalishaji wa teknolojia ya kisasa nchini China kilifikia zaidi ya asilimia kumi.
Kwa maelezo mengine ni kuwa, licha ya changamoto kubwa zilizotokana na kuenea kwa virusi cya corona duniani. China imefanikiwa kurejesha kiwango cha ustawi wa uchumi wake katika kiwango kilichokuwepo kabla ya kudhihiri janga la maradhi hayo na hivyo kuwa dola pekee kubwa duniani kukuza uchumi wake kwa asilimia chanya.
Profesa Eswar Prasad, mhadhiri wa masuala ya kibiashara katika Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani anasema kuhusu suala hilo kwamba: Uchumi wa China ungali unaendelea kukua kwa kasi na kwa kutegemea rekodi yake nzuri, uchumi huo utaendelea kuimarisha nafasi ya China kama injini muhimu ya ustawi wa uchumi duniani.
Mbali na mtalamu huyo wa Marekani, kanali ya habari ya televisheni ya CNBC imetoa ripoti ikiashiria ustawi wa pato jumla la ndani ya China na utabiri uliofanyika katika uwanja huo na kuandika kwamba: Tathmini ya karibuni inaonyesha kuwa nchi hiyo ya bara Asia itadhihiri kuwa nguvu kubwa ya kwanza kiuchumi duniani na hivyo kuipita Marekani haraka, kinyume na tabiri zinavyosema.