UN yaanzisha kampeni ya usambazwaji chanjo ya COVID-19 duniani kote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i67792-un_yaanzisha_kampeni_ya_usambazwaji_chanjo_ya_covid_19_duniani_kote
Umoja wa Mataifa umezindua kampeni ya kuhakikisha chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 zinapatikana kwa wote na popote pale duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2021 04:43 UTC
  • UN yaanzisha kampeni ya usambazwaji chanjo ya COVID-19 duniani kote

Umoja wa Mataifa umezindua kampeni ya kuhakikisha chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 zinapatikana kwa wote na popote pale duniani.

Kampeni hiyo iliyopewa jina la Ni Kwa Pamoja Tu, imezinduliwa Alhamisi kwa njia ya video na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye  amesema mwaka mmoja wa janga la Corona umesababisha wimbi la machungu. Ameongeza kuwa, "Virusi vimeua zaidi ya watu milioni 2.5 na kuacha mamilioni na madhara ya muda mrefu ya kiafya. Familia na uchumi vinaserereka. Hivi sasa kwa ahadi hii ya chanjo, tunaona nuru."

Amesema wanasayansi wamefanya maajabu, wametengeneza chanjo salama na thabiti katika muda ambao haujawahi kushuhudiwa, "sasa tuna mbinu ya kukomesha mwenendo wa COVID-19. Lakini ni nchi chache sana ndio zimepata idadi kubwa ya chanjo."

Kampeni hiyo inasisitiza umuhimu wa uratibu wa hatua za pamoja za kimataifa ili chanjo zifikie kila nchi kuanzia wahudumu wa afya hadi walio hatarini zaidi.

Katibu MKuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres akihutubu kwa njia ya video

Guterres amesema chanjo za COVID-19 lazima zionekane kuwa ni bidhaa ya umma duniani kote na kwamba hakuna nchi inaweza kukabili janga la sasa peke yake.

Amesema serikali na sekta za biashara lazima zigawane dozi za chanjo na teknolojia ili usambazaji wa chanjo uwe ni wa haraka.

Guterres amesema COVAX ambao ni mkakati wa chanjo ndio njia bora zaidi ya kufanikisha uwiano sawa wa kupata chanjo kwa kila mtu duniani, hivyo uwezeshwe. Ni kwa mantiki hiyo anasema, "Ni kwa pamoja tu tunaweza kulinda wahudumu wa afya na watu walio hatarini zaidi duniani. Ni kwa pamoja tu tunaweza kukwamua uchumi wetu. Ni kwa pamoja tu tunaweza kumaliza janga hili na kukwamuka. Na ndipo pamoja tunaweza kurejea tena katika vitu vyetu ambavyo tunavipenda."