UN yaikosoa Kenya kwa kupanga kufunga kambi za wakimbizi
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Kenya kufikiria upya mpango wake wa kufunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma.
Taarifa ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kutoka Geneva imesema kuwa, chombo hicho cha kimataifa kimetiwa wasi wasi mkubwa juu ya azma hiyo ya serikali ya Kenya ya kutaka kufunga kambi za wakimbizi, na kusisitiza kuwa mpango huo utaathiri wakimbizi zaidi ya laki 6 walioko katika kambi hizo.
Taarifa hiyo ya UN imeongeza kuwa, usalama wa maelfu ya wakimbizi wa Kisomali na raia wa Sudan Kusini kwa takriban robo karne umekuwa ukitegemea ukarimu wa Kenya na nia yake ya kutaka kuonyesha mfano bora katika eneo wa kutekeleza majukumu ya kimataifa.
Wakati huo huo, George Morara, Naibu Mwenyekiti wa Shirika la Taifa la Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya (KNCHR) amekosoa mpango huo wa serikali akisisitiza kuwa sio haki kuwarejesha wakimbizi hao sehemu walioikimbia huku akiitaka jamii ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo ya Afrika Mashariki kubeba mzigo wa kuwashughulikia wakimbizi hao.
Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF limetoa taarifa likisema kuwa kutekelezwa kwa uamuzi huo kutawaweka maelfu ya wakimbizi hatarini.
Kambi ya Dadaab ambayo iko umbali wa kilomita 100 hivi kutoka mpaka wa Somalia inahesabiwa kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ambapo kwa sasa nusu ya wakimbizi wanaoishi humo ni raia wa Somalia. Wakimbizi wa Kisomali wapatao 330,000 wanaishi katika kambi hiyo ilihali wengine 190,000 wanaishi katika kambi ya Kakuma.