Mar 24, 2021 02:48 UTC
  • Bangladesh yachunguza mkasa wa moto ulioua Waislamu 15 wa Rohingya

Serikali ya Dhaka imeanzisha uchunguzi kubaini kiini cha moto mkubwa uliotokea katika kambi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya katika wilaya ya Cox's Bazar nchini Bangladesh na kuua na kujeruhi mamia ya watu.

Johannes van der Klaauw, afisa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Bangladesh amesema kwa akali watu 15 wamepoteza maisha katika mkasa huo, mbali na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa.

Baadhi ya mashuhuda wanasema idadi ya watu waliofariki dunia kwenye mkasa huo ni zaidi ya ile iliyotangazwa na UNHCR na vyombo vya habari vya Bangladesh.

Afisa huyo wa UNHCR ameongeza kuwa, watu zaidi ya 400 hawajulikani walipo baada ya tukio hilo, na inahofiwa kuwa wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo na mabanda walikokuwa wanaishi wakimbizi hao kutoka Myanmar.

Amebainisha kuwa, wakimbizi zaidi ya 45,000 hawana pahala pa kuishi baada ya mahema na nyumba zao kuteketea kwa moto kwenye mkasa huo.

Athari za moto mkubwa uliotekeza makazi ya wakimbizi Warohingya nchini Bangladesh

Inaarifiwa kuwa, moto huo ulianzia kwenye kibanda kimoja katika kambi hiyo ya wakimbizi ya Balukhali, kusini mashariki mwa mji wa Cox's Bazar usiku wa kuamkia jana, na kisha ukaenea kwa kasi katika mahema na mabanda mengine ya wakimbizi hao.

Mnamo mwezi Agosti mwaka 2017, zaidi ya Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya walikimbilia Bangladesh kunusuru maisha yao na kutafuta hifadhi kutokana na vita na mauaji ya halaiki yaliyofanywa na jeshi la Myanmar na mabudha wenyewe misimamo ya kufurutu mpaka katika eneo wanaloishi la Rakhine; na hivi sasa wanaishi kwenye kambi za wakimbizi zilizoko kwenye mpaka wa Bangladesh.

Tags