Kuendelea mivutano kati ya China na Marekani
Licha ya kuwepo utabiri wa awali kwamba mivutano iliyokuwepo kati ya China na nchi za Magharibi na hasa Marekani katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump ingepungua pakubwa mara tu baada ya kuoondoka madarakani rais huyo na kuingia White House Joe Biden, lakini mivutano hiyo ingalipo bali imeongezeka hata zaidi.
Malalamiko dhidi ya chokochoko za Marekani katika Bahari ya China Kusini, kuchapishwa ripoti ya kila mwaka kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani, ulazima wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sisitizo la karibuni la viongozi wa China la kuitaka Marekani irejee kivitendo katika mapatano ya JCPOA, ni baadhi ya mambo ambayo yamethibitisha wazi katika siku za karibuni kwamba mivutano ya Beijing na Washington na vuilevile miji mikuu ya nchi nyingine za Magharibi kuhusu masuala mablimbali ya kimataifa ingalipo.
Akizungumzia suala hilo karibuni hivi, Cui Tiankai, Balozi wa China huko Marekani alisema kuwa Washington inapasa kuheshimu misingi iliyoainishwa katika Hati ya Umoja wa Mataifa kuhusu mahusiano ya nchi tofauti za dunia, iwapo inataka kuimarisha uhusiano wake wa kieneo na Beijing.
Akitoa radiamali yake kuhusu matamshi ya karibuni ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyesema kuwa Marekani haina nia ya kukabiliana na China lakini kwamba pande mbili hizo zina mashindano makali, Cui Tiankai amesema: 'Sisi hatuna tatizo lolote na mashindano huru na ya kiuadilifu. Lakini tatizo ni kwamba tukitazama mambo ambayo yametukia katika miaka iliyoppita kati ya China na Marekani, au tuseme baina ya Marekani na nchi nyingine za dunia, swali hili linaibuka moja kwa moja kwamba je, ni vipi mashindano ya aina hii yataitwa kuwa ni mashindano salama?
Matamshi ya Biden yanathibitisha wazi kwamba kwa uchache hataki kubadilisha siasa za hujuma ambazo mtangulizi wake Trump alizianzisha dhidi ya China.
Msimamo wa Rais Biden katika kukadhibisha kuwepo makabiliano na China na wakati huo huo kusisitiza juu ya kuendelea mashindano makali na nchi hiyo ya Asia, bila shaka umewakatisha tamaa wale waliokuwa na matumaini ya kutazamwa upya siasa za uhasama za Washington dhidi ya Beijing.
Sisitizo la China la kuendelea kuwa na msimamo huru katika ngazi za kimataifa kukiwemo kutofuata siasa za vikwazo za Marekani dhidi ya Iran na hasa baada ya kutiwa saini mkataba wa ushirikiano wa kistartejia wa miaka 25 kati ya Beijing na Tehran, uliotiwa saini Jumamosi katika safari ya Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China hapa mjini Tehran, ni jambo linaloashiria wazi kuendelea kupanuka pengo la tofauti katika uhusiano wa Marekani na China.
Marekani ambayo katika miongo kadhaa iliyopita imeiwekea Iran vikwazo vikali na vya kidhalimu kwa visingizio visivyo na msingi wowote, inaichukulia hatua ya karibuni ya Beijing ya kutiliana saini mkataba huo wa kistratejia kuwa ni hatua nyingine ya China ya kusambaratisha vikwazo na siasa zake za uadui dhidi ya Iran.
Pamoja na hayo, tunapasa kuzingatia kuwa tokea wakati Marekani ilipojitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na hatimaye kuzidishwa vikwazo dhidi ya Tehran, Iran ilianza kutekeleza siasa za kusimama imara katika kukabiliana na vikwazo hivyo vya kidhalimu jambo lililofanya vishindwe kufikia malengo yake, kama wanavyokiri wazi hilo Wamarekani wenyewe.
Kwa msingi huo, inatabiriwa kuwa uimarishwaji wa uhusiano wa China na Iran hadi kufikia kiwango cha uhusiano wa kistratijia, jambo ambalo limeikasirisha sana Marekani, utazidi kunoa makali ya mashindano ya Marekani na China kama alivyoashiria suala hilo Biden mwenyewe.
Watawala wa White House wana wasi wasi kwamba huenda China na Iran zikishirikiana na nchi nyingine za eneo ikiwemo Russia katika kuunda muungano mpya wenye nguvu kubwa kieneo na hivyo kuhatarisha ubabe wa Marekani na mipango yake ya kibeberu katika eneo.
Inaonekana kuwa siasa za hujuma, upande mmoja na za mabavu za White House katika kuamiliana na nchi nyingine za dunia na miungano ya kieneo na kimataifa zimeipelekea Marekani, kuanza kudhoofika kimataifa kinyume na ilivyokuwa ikidhani kwamba jambo hilo lingeiwezesha kupata nguvu zaidi na hivyo kuondelea kuikandamiza dunia.