Maelfu ya watoto wahajiri wanashikiliwa katika mazingira ya kuogofya Marekani
(last modified Fri, 28 May 2021 12:19:07 GMT )
May 28, 2021 12:19 UTC
  • Maelfu ya watoto wahajiri wanashikiliwa katika mazingira ya kuogofya Marekani

Watoto zaidi ya 4,300 ambao hawana wazazi wala wasimamizi na ambao waliingia nchini Marekani wakitokea Mexico wanazuiliwa katika mazingira ya kutisha jimboni Texas.

Duru za habari zinaarifu kuwa, watoto hao wahajiri ambao wana umri kati ya miaka 13 na 17 wamezuiliwa katika kituo cha muda kilichoko katika kambi ya kijeshi katika mji wa El Paso kwa wiki kadhaa sasa.

Inaarifiwa kuwa, watoto hao wahajiri wanazuiliwa katika kituo cha muda kilichoundwa wiki tisa zilizopita na Wizara ya Afya na Hudumu za Kibinadamu ya Marekani.

Wahudumu na watetezi wa haki za watoto kambini hapo wanasema kituo hicho hakina usimamizi mzuri na watoto wanaozuiliwa hapo wanapitia kipindi kigumu.

Watoto wahajiri wanaozuiliwa katika mazingira magumu US

Baadhi ya wahudumu hao wamenukuliwa na gazeti la El Paso Times wakikitaja kituo hicho jumba gofu au kaburi la watu walio hai. Wanasema baadhi ya watoto wamezuiliwa kituoni hapo kwa zaidi ya siku 40, jambo ambalo halikubaliki.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, mahakama moja nchini Marekani ilitaka kufanyika uchunguzi kuhusu watoto waliohajiri nchini humo na kisha kutenganishwa na familia zao. Mahakama hiyo iliiagiza kamati teule ya uchunguzi iendelee kufanya uchunguzi ili kuwapata wazazi wa watoto 628 ambao walitengenishwa katika mpaka wa Mexico na nchi hiyo kwa amri ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati huo Donald Trump.