WHO: COVID-19 kuua watu 236,000 zaidi Ulaya kufikia Disemba
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74136-who_covid_19_kuua_watu_236_000_zaidi_ulaya_kufikia_disemba
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa, yumkini watu wengine 236,000 wakaaga dunia kutoka na maradhi ya COVID-19 barani Ulaya kufikia Disemba Mosi mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 31, 2021 09:14 UTC
  • WHO: COVID-19 kuua watu 236,000 zaidi Ulaya kufikia Disemba

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa, yumkini watu wengine 236,000 wakaaga dunia kutoka na maradhi ya COVID-19 barani Ulaya kufikia Disemba Mosi mwaka huu.

Hans Kluge, Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya amesema, bara hilo lilishuhudia ongezeko la asilimia 11 la vifo vya Corona wiki iliyopita.

Amesema nchi 33 kati ya 53 wanachama wa Umoja wa Ulaya, zimerekodi ongezeko la kesi na vifo vya Corona kwa asilimia 10 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya ameongeza kuwa, maambukizi ya virusi vya Corona aina ya Delta yamepelekea kuongezeka pakubwa idadi ya wagonjwa na wahanga wa ugonjwa wa COVID-19 katika nchi za bara hilo.

Corona Ulaya

Kadhalika amesema kulegezwa bila mpangilio sheria kali za kudhibiti msambao wa maradhi hayo pia kumechangia kuongezeka kwa idadi na kesi na vifo barani humo.

Aidha amelaumu kupungua kwa asilimia 16 utoaji wa chanjo ya Corona ndani ya wiki sita zilizopita barani Ulaya kwa ongezeko hilo.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, watu zaidi ya milioni 64 wameambukizwa kirusi cha corona barani Ulaya, huku bara hilo likinakili vifo milioni 1.3 vya maradhi hayo kufikia sasa.