Kimbunga Ida chaua watu 61 Marekani, maelfu wapoteza makazi yao
Kimbunga cha Ida kilichotokea katika majimbo kadhaa ya kaskazini mashariki mwa Marekani kimeua makumi ya watu na kuwafanya maelfu ya wengine wapoteze makazi yao.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, kimbunga hicho kikali kimeua watu 61 kufikia jana Ijumaa. Jimbo la New Jersey ndilo limeathirika zaidi na makali ya kimbunga hicho, baada ya watu 25 kupoteza maisha.
Meya wa jiji la New York, Bill de Blasio amesema watu 13 wameaga dunia kutokana na kimbunga hicho mjini hapo. Vifo vingine vimeripotiwa katika majimbo ya Connecticut, Maryland, na Pennsylvania.
Habari zaidi zinasema kuwa, usafiri na huduma za umeme na mawasiliano pia zimekatika kutokana na Kimbunga Ida katika majimbo ya kaskazini mashariki.
Mbali na hasara za nafsi na mali, kimbunga hicho ambacho kimesababisha mvua kubwa na mafuriko, kimesababisha kukatika umeme wa malaki ya nyumba na vituo na maeneo ya kibiashara katika majimbo ya New York na New Jersey.
Siku ya Alkhamisi, Rais Joe Biden a Marekani alitangaza hali ya hatari katika majimbo hayo mawili, kufuatia athari hasi za Kimbunga Ida, kinachokwenda kwa kasi kubwa.