Kubadilika siasa za nje za Saudia kuhusu uhusiano na madola makubwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74584-kubadilika_siasa_za_nje_za_saudia_kuhusu_uhusiano_na_madola_makubwa
Hatua ya Saudi Arabia kufutilia mbali safari ya waziri wa ulinzi wa Marekani na wakati huo huo kumkaribisha mjini Riyadh mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Russia Duma, ni jambo linaloashiria kwamba Saudia imeamua kuimarisha uhusiano wake na madola mengine yenye nguvu duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2021 21:56 UTC
  • Kubadilika siasa za nje za Saudia kuhusu uhusiano na madola makubwa

Hatua ya Saudi Arabia kufutilia mbali safari ya waziri wa ulinzi wa Marekani na wakati huo huo kumkaribisha mjini Riyadh mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Russia Duma, ni jambo linaloashiria kwamba Saudia imeamua kuimarisha uhusiano wake na madola mengine yenye nguvu duniani.

Je, ni kwa nini Saudia ikachukua uamuzi wa kufutilia mbali wakati huu safari ya wazairi wa ulinzi wa Marekani?

Bila shaka hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kukasirishwa Saudia na siasa za serikali ya Washington. Katika kipindi cha kampeni zake za uchaguzi wa rais, Rais Joe Biden wa Marekani aliukosoa vikali utawala wa ukoo wa Saud huko Saudia. Wakati huo, wachambuzi na weledi wa mambo walitabiri kwamba misimamo iliyochukuliwa na Biden katika kampeni zake za uchaguzi ilikuwa na maana ya kusitishwa kwa muda, kipindi cha uhusiano mzuri uliokuwepo baina ya nchi mbili.

Baada ya kushinda uchaguzi wa Marekani, Biden alichukua hatua ya kuliondoa kundi la Ansarullah la Yemen katika orodha yake ya makundi yanayotuhumiwa kuunga mkono ugaidi, kuhuisha faili la uchunguzi wa kifo cha Jamal Khashoggi, mwandishi na mkosoaji mkuu wa siasa za watawala wa Saudia, aliyeuawa katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul Uturuki, na wakati huo huo kutangaza hadharani sehemu ya uchunguzi uliokuwa umefanyika katika uwanja huo na kuhifadhiwa kuwa siri kubwa.

Saudia ilikuwa na uhusiano mzuri sana na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani

Hata kama Marekani haikuchukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya utawala wa Aal Saud katika uwanja huo, lakini kwa kufichua ukiukaji wake wa haki za binadamu iligusa na kuanika peupe nukta muhimu ya udhaifu wake na hivyo kutoa mashinikizo makubwa ya kisiasa dhidi ya utawala huo katika ngazi za kimataifa.

Mbali na hayo, hivi karibuni Rais Biden alitoa amri ya kuchunguzwa upya nyaraka zinazohusiana na mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani na kuchapishwa hadharani nyaraka hizo. Kwa kutilia maanani kwamba raia wa Saudia walihusika moja kwa moja katika mashambulizi hayo, suala hilo limeongeza hasira ya watawala wa Saudia dhidi ya serikali ya Washington.

Kwa maneno mengine ni kuwa, watawala wa Saudia wamefikia uamuzi kwamba kwa sasa hakuna heshima inayoonekana katika uhusiano wa pande mbili na kwamba Washington haizingatii tena maslahi ya Riyadh katika uhusiano huo.

Katika uwanja huo, Sattam bin Khalid bin Nasser Al Saud, mmoja wa wanawafalme wa Saudia aliashiria karibuni katika ukurasa wake wa Twitter suala la kufutiliwa mbali safari ya Lloyd Austin Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Saudia na kusema nchi hiyo ni nchi muhimu ambayo haitakubali kuamrishwa na nchi yoyote na kwamba itashirikiana na nchi nyingine kwa msingi wa kudhaminiwa maslahi ya kitaifa na kuheshimiana pande mbili.

Vile vile Alkhamisi, Turki al-Faisal, mkuu wa zamani wa idara ya usalama ya Saudi Arabia alikosoa hatua ya Marekani ya kuondoa Saudia ngao ya makombora ya Patriot na kusema  licha ya kuwa Saudia inafadhilisha msaada wa Marekani lakini itatafuta msaada wa nchi nyingine katika kuimarisha ulinzi wake wa anga katika kukabiliana na mashambulizi ya Yemen.

Turki al-Faisal

Matamshi hayo ya maafisa wa Saudia yanathibitisha wazi kwamba hitilafu na mivutano katika uhusiano wa nchi hiyo na Marekani imeisukuma ukutani Saudia na kuifanya ichukue  uamuzi wa kuanzisha uhusiano na mahasimu wa Marekani, na hasa Russia. Hata kama hatua hiyo inaweza kutathminiwa kuwa imechukuliwa kwa ajili ya kutoa mashinikizo dhidi ya Washington ili isitishe mashinikizo yake dhidi ya Riyadh, lakini wakati huo huo, ni jambo linaloonyesha kuwa watawala wa Saudia wamefikia natija kwamba kuitegemea Marekani kupita kiasi si tu hakudhamini maslahi ya taifa hilo bali kunayadhuru pia.