Trump: Hakuna njia nyingine isipokuwa mimi nigombee urais mwaka 2024
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74636-trump_hakuna_njia_nyingine_isipokuwa_mimi_nigombee_urais_mwaka_2024
Aliyekuwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema alipoulizwa kama atagombea urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024 au la kwamba, hakuna njia nyingine isipokuwa hiyo.
(last modified 2026-05-05T14:43:53+00:00 )
Sep 14, 2021 02:47 UTC
  • Trump: Hakuna njia nyingine isipokuwa mimi nigombee urais mwaka 2024

Aliyekuwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema alipoulizwa kama atagombea urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024 au la kwamba, hakuna njia nyingine isipokuwa hiyo.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na chaneli ya televisheni ya Fox News, Trump amezungumzia mipango yake kwa ajili ya kugombea urais katika mwaka 2024 na akabainisha kwamba, "hali imefikia mahala ambapo hakuna njia nyingine isipokuwa hii. Hili ni jambo la kuaibisha."

Rais huyo wa zamani wa Marekani amegusia pia utekelezaji wa mchakato uliosimamiwa na serikali ya Joe Biden wa kuwaondoa askari na zana za kijeshi za Marekani nchini Afghanistan na akautaja kuwa ni "jambo la kuaibisha zaidi katika historia ya Marekani".

Trump amedai: "wakati unapoitazama Afghanistan na matukio yaliyotokea huko unaona baadhi ya watu wameuawa bila ya sababu. Kwa kweli wameuawa bila ya sababu."

Joe Biden

Hata kabla ya kuuawa askari wa Marekani, rais Joe Biden aliandamwa na lawama na ukosoaji kuhusuiana na matukio ya Afghanistan.

Wabunge wa Kongresi ya Marekani, wakiwemo waitifaki wa Biden wa chama cha Democratic, wameonyesha kutoridhishwa hata kidogo na matukio ya Afghanistan na kusisitiza kuwa wanakusudia kufanya uchunguzi kuhusu sababu za kutokea hali mbaya iliyoshuhudiwa nchini humo.

Hata hivyo rais Joe Biden wa Marekani ametetea uamuzi aliochukua kuhusu Afghanistan, ijapokuwa amejaribu pia kujivua na dhima ya matukio yanayojiri hivi sasa nchini humo na kuwabebesha watu wengine.../