'Kuua raia mjini Kabul kumeonyesha udhaifu wa kiintelijensia wa Marekani'
(last modified Mon, 20 Sep 2021 11:22:01 GMT )
Sep 20, 2021 11:22 UTC
  • 'Kuua raia mjini Kabul kumeonyesha udhaifu wa kiintelijensia wa Marekani'

Mchambuzi wa zamani wa masuala ya usalama katika wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon amesema, kukiri makamanda wa jeshi la Marekani kwamba walifanya shambulio kimakosa katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kuua raia wa nchi hiyo kumeonyesha udhaifu wa kiintelijensia wa Washington.

Michael Maloof amesema, kwa kiwango fulani, ni jambo lisilo la kawaida kwa makamanda wa kijeshi wa Marekani kukiri kuwa wamefanya makosa katika mashambulio waliyofanya.

Maloof ameendelea kueleza kwamba, makamanda hao wa jeshi la Marekani wamezoea kwa miaka kadhaa sasa kushambulia kwa makombora nchini Syria na kaskazini mwa Iraq na katu hawajawahi kukiri kuhusu mashambulio waliyofanya kimakosa katika maeneo hayo.

Mchambuzi huyo wa zamani wa masuala ya usalama katika wizara ya ulinzi ya Marekani amesisitiza kwa kusema: "tumeshuhudia jenerali wa jeshi la Mareani akikubali kubeba dhima ya shambulio la kimakosa la hivi karibuni nchini Afghanistan na hata kupendekeza kutolewa fidia kwa familia za waathirika, lakini hatua hiyo haiwezi kuwarejesha tena watoto na watu wazima waliouawa."

Jenerali Frank McKenzie (aliyevaa sare za jeshi)

Siku ya Ijumaa, kamanda wa vikosi vya kigaidi vya jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi CENTCOM, Jenerali Frank McKenzie alitangaza mjini Wshington kwamba, uchunguzi wa kijeshi kuhusu shambulio la anga la tarehe 29 Agosti lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya nchi hiyo mjini Kabul umeonyesha kuwa, raia 10 wakiwemo watoto saba waliuawa katika shambulio hilo; na kuna uwezekano dereva na gari lililolengwa katika shambulio hilo halikuwa tishio wala halikuwa la kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) kama ilivyodhaniwa.../