WHO yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya Afghanistan tangu Taliban washike madaraka
-
Tedros Adhanom
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuhusu hali ya Afghanistan tangu kundi la wapiganaji wa Taliban liliposhika madaraka ya nchi hiyo na kutangaza kuwa Afghanistan inakaribia kutumbukia katika maafa ya binadamu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom ametoa taarifa baada tu ya kurejea Geneva akitokea Kabul na kusema kwamba mfumo wa afya wa Afghanistan unakaribia kusambaratika na kwamba iwapo hakutachukuliwa hatua za dharura nchi hiyo itatumbukia katika maafa makubwa ya binadamu.
Katika taarifa hiyo Adhanom amesisitiza udharura wa kukidhiwa mahitaji ya Afghanistan na kuongeza kuwa, vituo vingi vya afya nchini humo vimefungwa na kwamba kwa sasa ni asilimia 17 tu ya vituo hivyo ndiyo inayofanya kazi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alikuwa nchini Afghanistan kwa ajili ya kuchunguza hali ya kiafya ya nchi hiyo.
Kundi la Taliban lilingia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul tarehe 15 Agosti mwaka huu baada ya serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ashraf Ghani kusambaratika. Kuingia Taliban mjini Kabul kulihitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na washirika wake wa NATO nchini Afghanistan.