ICC kuchunguza tuhuma za jinai zilizofanywa na Taliban na Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75152-icc_kuchunguza_tuhuma_za_jinai_zilizofanywa_na_taliban_na_daesh
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa, kipaumbele cha taasisi hiyo kuhusu uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanyika nchini Afghanistan sasa kitaelekezwa kwa makundi ya Taliban na Daesh.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Sep 28, 2021 07:17 UTC
  • ICC kuchunguza tuhuma za jinai zilizofanywa na Taliban na Daesh

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa, kipaumbele cha taasisi hiyo kuhusu uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanyika nchini Afghanistan sasa kitaelekezwa kwa makundi ya Taliban na Daesh.

Bila ya kuashiria hata kidogo jinai za kivita na dhidi ya binadamu zilizofanywa na Marekani nchini Afghanistan, Mwendesha Mashtaka mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Karim Khan amesema kuwa, taasisi hiyo itaanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma za jinai zilizofanywa na Taliban na Daesh huko Afghanistan.

 Itakumbukwa kuwa hatua ya mahakama ya ICC ya kuanzisha uchunguzi wa jinai za kivita za wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan ilivuruga uhusiano wa taasisi hiyo na serikali ya Washington katika kipindi cha utawala wa Donald Trump. 

Wakati huo serikali ya Marekani ilimuwekea vikwazo aliyekuwa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda na jaji aliyekua akishughulikia faili hilo, Karim Khan. 

Baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001 katika miji ya New York na Washington, Marekani iliivamia na kuishambulia nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuiondoa madarakani serikali ya kundi la Taliban ambalo inalituhumu kuwa lilishirikiana na al Qaida katika mashambulizi ya Septemba 11. 

Maelfu ya raia wa Afghanistan wameuawa katika mashambulizi ya Marekani, NATO

Takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, madawa ya kulevya, uharibifu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Katika kipindi hicho wanajeshi 2,448 wa Marekani wameuawa wakiwa vitani, na vilevile wanajeshi 1144 wa shirika la NATO wameuawa katika vita hivyo.