Mahakama ya ICC yafumbia jicho jinai zilizofanywa na Marekani nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75166-mahakama_ya_icc_yafumbia_jicho_jinai_zilizofanywa_na_marekani_nchini_afghanistan
Licha ya uhalifu mkubwa na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani nchini Afghanistan katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) sasa inakusudia kuweka kando uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Marekani na NATO nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 28, 2021 12:09 UTC
  • Mahakama ya ICC yafumbia jicho jinai zilizofanywa na Marekani nchini Afghanistan

Licha ya uhalifu mkubwa na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani nchini Afghanistan katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) sasa inakusudia kuweka kando uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Marekani na NATO nchini humo.

Mwendesha Mashtaka mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Karim Khan amesema, mahakama hiyo inataka kupata kibali cha kuanza uchunguzi wa jinai za kivita uliofanywa na wapiganaji wa Taliban na makundi mengine ya waasi nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, uchunguzi huo hautahusu jinai na uhalifu wa kivita uliofanywa na Wamarekani.

Mwezi Machi mwaka 2020 Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilianzisha uchunguzi kuhusu jinai na uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan baina ya mwaka 2003 na 2014. Suala hilo lilikabiliwa na upinzani mkali wa rais aliyeondoka madarakani wa Marekani, Donald Trump ambaye mwaka 2017 aliwawekea vikwao maafisa wa mahakama hiyo. 

Katika kipindi cha miongo miwili ya kuwepo huko Afghanistan wanajeshi wa Marekani walifanya jinai na uhalifu mwingi na wa kutisha. Idadi kubwa ya raia wasio na hati wa Afghanistan waliuawa kwa mabomu na mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani. Vilevile watoto wengi waliuawa au kutumiwa vibaya na Wamarekani. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika kipindi cha miezi 30 ya kufikia mwezi Juni mwaka huu pekee watoto 6,320 wa Afghanistan wameuawa au kujeruhiwa wakati nchi hiyo ikikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani na washirika wake. 

Maelfu ya watoto wa Afghanistan wameuawa katika mashambulizi ya Marekani

Siku chache zilizopita pia askari mmoja wa Marekani alifichua kuwa, wanajeshi wa nchi yake walikuwa wakiwatumia watoto wa Kiafghani kwa ajili ya kusafisha maeneo yaliyotengwa mabomu. Sajenti Jeff Cork ambaye alipelekwa Afghanistan mwaka 2010 akiwa kwenye timu ya radiamali ya haraka ya jeshi la Marekani anasema, watoto waliokuwa na umri wa chini ya miaka 10 wa Afghanistan walitumiwa kusafisha maeneo na mitaa iliyoshukiwa kuwa na mabomu ya kutegwa ardhini kwa njia ya kuwarubuni kwa kurusha chokoleti au wanasesere katika maeneo hayo.  

Katibu Mkuu wa chama cha Ustawi wa Kitaifa nchini Afghanistan, Muhammad Hassan Jaafari anasema: "Wamarekani wameharibu nchi hii na kuifanya magofu, na vilevile wamebakisha nyuma makundi yanayofanyakazi kwa niaba yao nchini Afghanistan.”

Uhalifu, jinai za kivita na ukiukaji wa haki za binadamu wa Marekani nchini Afghanistan ulifanyika chini ya mwavuli na kaulimbinu ya kutoa misaada ya kibinadamu na kuimarisha demokrasia! Viongozi wa Marekani siku zote wamekuwa wakijitokeza mbele ya vyombo vya habari ya kudai kuwa, majeshi ya nchi hiyo na washirika wake yamepelekwa Afghanistan kwa ajili ya kutoa misaada ya kibinadamu, kujenga demokrasia na kupambana na ugaidi. Hata hivyo ukweli ni kuwa, nchi hizo za Magharibi zenyewe zimekuwa zikiyafadhili na kuyasaidia makundi ya kigaidi na kustawisha biashara ya dawa za kulevya kwa malengo yao wenyewe.

Wanajeshi wa Marekani wakilinda mashamba ya kilimo cha mpopi unaotumiwa kuzalisha dawa za kulevya

Dakta Abdulatif Nazari ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu nchini Afghanistan anasema: "Wamarekani hawakuja hapa kwa ajili ya kujenga na kustawisha taifa hili, bali kwa ajili ya kufuatilia na kudhibiti nyendo za nchi za kanda hii hususan wapinzani wa serikali ya Washington. Marekani imetumia kisingizio cha uhuru wa kusema, haki za binadamu, kuijenga Afghanistan, kusaidia vyombo vya habari na kadhalika kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya kistratijia na si vinginevyo.”

Marekani iliivamia Afghanistan kwa kaulimbiu ya kuimarisha demokrasia na haki za binadamu. Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, uzalisha wa madawa ya kulevya, uharibifu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Sasa na kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika nchi hiyo na kuondoka kwa madhila na fedheha majeshi ya Marekani huko Afghanistan, viongozi wa Washington wanafanya mikakati ya kujaribu kufunika na kuficha dhulma na ukatili mkubwa uliofanywa na wajashi wa nchi hiyo dhidi ya Waafghani.

Mashinikizo yanayofanywa dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa ajili ya kupotosha faili la jinai za kivita zilizofanywa na Marekani huko Afghanistan yanawea kutathminiwa katika mkondo huu.