Kupamba moto mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76792-kupamba_moto_mgogoro_wa_wakimbizi_barani_ulaya
Kwa mara nyingine tena, wimbi la wakimbizi wanaomiminika kwenye mipaka ya nchi za Ulaya limeongezeka na kuwa mgogoro mkubwa. Nchi za Ulaya zimeamua kufunga mipaka yao ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi wapya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 11, 2021 10:40 UTC
  • Kupamba moto mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya

Kwa mara nyingine tena, wimbi la wakimbizi wanaomiminika kwenye mipaka ya nchi za Ulaya limeongezeka na kuwa mgogoro mkubwa. Nchi za Ulaya zimeamua kufunga mipaka yao ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi wapya.

Nchi za mashariki mwa Ulaya ndizo zilizo na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kiasi kwamba viongozi wa Poland wamesema wana wasiwasi mkubwa na mgogoro huo. Viongozi hao wameamua kuweka wanajeshi 12,000 kwenye mipaka yake ili kuzuia kuingia nchini humo wakimbizi kutoka nje.

Mikanda ya video iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii inaonesha kuwa, mamia ya wakimbizi wamejikusanya hivi sasa kwenye mipaka ya Poland. Katika wiki za hivi karibuni pia, bunge la nchi hiyo liliidhinisha kujengwa uzio mkubwa na wa kudumu kwenye mipaka yake ili kuzuia wakimbizi kuingia nchini humo. 

Moja ya sababu za kushuhudiwa ongezeko hilo la wakimbizi barani Ulaya katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni ni mabadiliko ya kisiasa yaliyojitokeza kimataifa kama vile kudhibitiwa Afghanistan na kundi la Taliban. Wengi wa wakimbizi hao wameamua kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kupata usalama na maisha bora. Hata hivyo nchi hizo za Ulaya zimeamua kufunga mipaka yao kwa hofu ya kuingia kwenye mgogoro mpya wa wakimbizi kama ule wa mwaka 2016.

Wakimbizi wanahatarisha mno maisha yao kujaribu kufika barani Ulaya

 

Katika upande mwingine, mivutano ya kisiasa baina ya Umoja wa Ulaya na Belarus imepelekea suala la wakimbizi kutumiwa kama silaha za kisiasa dhidi ya tawala za nchi nyingine. Katika miezi ya hivi karibuni, nchi za Poland, Lithuania, Latvia na Umoja wa Ulaya zimesikika zikiituhumu Belarus kuwa inawasukuma kwa makusudi wakimbizi; upande wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Umoja huo unaituhumu Belarus kuwa imeanzisha vita vya mbinu na suhula mchanganyiko dhidi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kwamba Brussels inaamini kuwa, vita hivyo vimeanzishwa kwa makusudi na Belarus ili kulipiza kisasi cha vikwazo vilivyowekwa na umoja huo dhidi ya Minsk katika miezi ya hivi karibuni. Hata hivyo serikali ya Belarus imepinga vikali madai hayo.

Kwa upande wake, gazeti la Daily Mail limeandika katika toleo lake la mtandaoni kwamba, tangu viliopoanza vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Minsk, idadi ya wakimbizi wameongezeka katika mpaka wa kilomita 670 wa Belarus na Umoja wa Ulaya. Mwaka huu pia zaidi ya wakimbizi elfu nne na 100 wameingia nchini Lithuania likiwa ni mara 50 zaidi ikilinganishwa na mwaka jana 2020. 

Vyombo vya habari vya Ujerumani navyo vimeripoti hali mbaya waliyo nayo wakimbizi kutokana na sheria kali za Poland katika mpaka wake na Belarus. Kwa mujibu wa vyombo hivyo, hali ya wakimbizi ni janga la kibinadamu. Wakimbizi hao wanapitisha siku zao, usiku na mchana katika baridi hali ambayo ni daraja nane chini ya sifuri, wakiwa na watoto wadogo, bila ya chakula wala hata mahema ya kujihifadhia. Hawana hata huduma za matibabu huku taasisi za misaada bali hata waandishi wa habari nao hawaruhusiwi kuonana na wakimbizi hao.

Poland imeweka wanajeshi 12,000 kuzuia wakimbizi bila ya kujali hali za watoto wadogo wanaopitisha siku zao kwenye baridi kali kupindukia

 

Mazingira magumu sana waliyo nayo wakimbizi hivi sasa katika mipaka ya Ulaya hasa kwenye mipaka ya Poland, hayastahamiliki. Shirika la Amnesty International limeitaka Poland kuondoa sheria zake kali na kuruhusu angalau misaada ya kibinadamu iwafikie wakimbizi hao.

Nchi za Ulaya zimeamua kufuata siasa kali na zisizo za kibinadamu dhidi ya wakimbizi licha ya nchi hizo kudai kuwa ni viranja wa kutetea haki za binadamu, kupenda kusaidia watu na kuchunga masuala ya uhuru na kila mmoja kuwa na haki sawa na mwengine. Hivi sasa nchi hizo za Ulaya zinashutumiwa kwa kuvunja vibaya haki za wakimibzi na kutoruhusu angalau waandishi wa habari waakisi masaibu yao.

Mwandishi mmoja na mtafiti wa masuala ya Bunge la Ulaya ameandika: Ulaya imeshindwa kutekeleza ahadi zake kuhusu haki za binadamu kama ambavyo imeshindwa pia kuzuia na kuongezeka ukatili dhidi ya binadamu.

Ni ukweli usiopingika kwamba, wakimbizi barani Ulaya wanaishi katika mazingira magumu sana. Hali hiyo imefichua uongo wa madai ya nchi za Ulaya wa kupenda ubinadamu, uhuru na haki za kila mtu. Nchi hizo za Ulaya zimethibitisha kivitendo kuwa zinashughulishwa tu na maslahi yao na hata wakimbizi wanatumiwa vibaya na nchi hizo kwa maslahi hayo binafsi tu.