Mauaji mengine ya kutisha gerezani yaripotiwa Ecuador
Wafungwa wasiopungua 68 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika ghasia zilizotokea kwenye gereza moja nchini Ecuador.
Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Ecuador imesema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumamosi kuwa, ghasia hizo za umwagaji damu zimetokea katika Gereza la Penitenciaria del Litoral viungani mwa jiji la Guayaquil katika mkoa wa Guayas.
Watu wanaoishi karibu na gereza hilo wamesema milio ya risasi na miripuko ilisikika kwa saa kadhaa kwenye gereza hilo, wakati wa kujiri makabiliano hayo.
Gereza hilo imekuwa eneo la mapigano ya umwagaji damu kati ya magenge yanayotaka kudhibiti jela ya gereza hilo katika miezi ya hivi karibuni.

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, wafungwa wasiopungua 119 waliuawa na wengine karibu 80 walijeruhiwa katika ghasia zingine zilizotokea kwenye gereza hilo.
Mapigano kama hayo yalitokea pia Februari na Julai mwaka huu wa 2021 katika magereza mbalimbali kote nchini humo na watu wasiopungua 101 waliuawa katika ghasia hizo.
Takwimu zinaonesha kuwa, wafungwa wasiopungua 300 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa katika ghasia za namna hiyo, kutokana na mfumo mbovu wa magereza ya nchi hiyo.