Sisitizo la Iran na Uturuki la kustawisha mashirikiano baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/world-i77854-sisitizo_la_iran_na_uturuki_la_kustawisha_mashirikiano_baina_yao
Marais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wamesisitiza kustawisha mashirikiano baina ya nchi mbili katika uga wa uchumi na kupambana na ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2021 04:00 UTC
  • Sisitizo la Iran na Uturuki la kustawisha mashirikiano baina yao

Marais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wamesisitiza kustawisha mashirikiano baina ya nchi mbili katika uga wa uchumi na kupambana na ugaidi.

Katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Recep Tayyip Erdogan, Seyyid Ibrahim Raisi ametilia mkazo umuhimu wa uhusiano wa Tehran na Ankara katika nyanja za uchumi na biashara na akeleza kwamba, kupitia kikao cha pamoja kitakachofanyika mjini Tehran, karibuni hivi suala la kustawisha mashirikiano baina ya nchi mbili litaingia kwenye awamu mpya.

Marais Raisi wa Iran na Erdogan wa Uturuki

Kwa upande wake, Rais wa Uturuki naye pia amesema mashirikiano kati ya nchi mbili yana umuhimu, hususan katika uga wa uchumi, na akabainisha kuwa, hivi sasa fikra inayotawala ni ya kustawishwa mashirikiano ya pamoja kati ya nchi za eneo; na kwamba safari na mashauriano yaliyofanywa hivi karibuni ni ishara ya kufanikiwa fikra na wazo hilo.

Halikadhalika, Erdogan amesisitiza kufanyika vikao vya pamoja vya ushirikiano kati ya Tehran na Ankara na akasema, katika safari yake ijayo hapa mjini Tehran, uhusiano wa nchi mbili utaingia katika awamu mpya ya ustawi.

Kwa sababu ya masuala ya kijiopolitiki, Iran na Uturuki zina mambo kadhaa yanayoziunganisha kihistoria, kiutamaduni, kimuundo wa idadi ya watu na katika maliasili; na zinahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye taathira kubwa katika eneo; hivyo kustawishwa zaidi uhusiano wa nchi mbili ni jambo muhimu kwa ajili ya kuleta uthabiti na kudhamini amani na usalama wa eneo hili.

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inazipa kipaumbele cha kwanza nchi jirani na za Kiislamu katika sera zake za nje, matatizo mengi yaliyopo hivi sasa katika eneo likiwemo la ugaidi yanatokana na uingiliaji wa madola ya nje ya eneo na uwepo wa madola hayo ajinabi na ya kigeni; na utatuzi wa matatizo hayo unahitaji juhudi na ushirikiano wa pamoja wa nchi za eneo hili.

Ni kwa msingi huo, katika miezi ya karibuni, viongozi wa Iran na Uturuki wamekutana na kufanya mashauriano zaidi kuhusiana na matukio ya kikanda na kimataifa na kutilia mkazo udharura wa kupatikana uthabiti, usalama na utulivu katika eneo la Asia Magharibi sambamba na kupewa umuhimu siasa na sera za ujirani mwema na kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili.

Rais Raisi  wa Iran (kushoto) na Rais Erdogan wa Uturuki

Wakati marais wa Iran na Uturuki walipokutana pembeni ya kikao cha Jumuiya ya Uchumi ya ECO kilichofanyika mjini Eshq-Abad, Turkmenistan, Erdogan alisisitiza kuwa, kwa mtazamo wa nchi yake, kustawisha na kuimarisha mashirikiano ya pande mbili na ya kikanda na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo la dharura na akaongezea kwa kusema: "Tunao uwezo wa kuongeza kwa kasi kubwa kiwango cha uhusiano wa nchi mbili, hasa katika sekta za kiuchumi."

Tukiuangalia uhusiano wa Iran na Uturuki tutabaini kuwa, licha ya tofauti za kisiasa na ushindani wa kieneo, nchi hizi mbili jirani ambazo zina mpaka wa pamoja wenye urefu wa karibu kilomita 500 zinaamini kuwa, kudumisha uhusiano wa kirafiki na kustawisha uhusiano wa kiuchumi ni jambo lenye udharura. Kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Uturuki ni takribani dola bilioni 70, lakini kimepungua katika miaka ya karibuni na kufikia dola bilioni tisa kutokana na msambao wa virusi vya corona na vikwazo haramu na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran.

Lenye maslahi kwa Iran na Uturuki ni nchi mbili hizi muhimu katika eneo hili kustawisha mashirikiano ya kikanda na ya pande mbili, jambo ambalo litathibiti na kufanikishwa kwa uzito mkubwa zaidi baada ya kukamilika hati ya mashirikiano ya muda mrefu baina ya nchi mbili. Yamkini hati hiyo itasainiwa na viongozi wa nchi mbili katika safari ijayo ya Rais wa Uturuki  hapa mjini Tehran.

Hivi sasa kuna aina kwa aina za fursa katika nchi mbili kwenye sekta za viwanda, kilimo, huduma na utalii, mafuta, gesi na petrokemikali ambazo zinaweza kutiliwa mkazo katika uandaaji wa hati hiyo.

Barsam Mohammadi, mtaalamu wa masuala ya eneo ana haya ya kunena kuhusiana na suala hilo: "Hati ya mashirikiano ya muda mrefu baina ya Iran na Uturuki itakuwa na taathira chanya katika kubuni uwezo na fursa mpya na uelewa wa pamoja wa maslahi ya kitaifa na ya kikanda kupitia uratibu wa mikakati mikuu katika uhusiano wa nchi mbili".../