Kufanyika mkutano wa umoja wa Kiislamu nchini Pakistan
Mkutano wa umoja wa Kiislamu umefanyika katika mji wa Lahore, Pakistan kwa kuhudhuriwa na Hujjatul Islam Wal muslimin Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Baraza la Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu na Sirajul-Haq, Kiongozi wa chama cha Jaamatul-Islami cha Pakistan.
Ulazima wa kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa pamoja, kuandaa mazingira yasiyotawaliwa na mizozano wala kuvunjiana heshima ili kuweza kufanyika mazungumzo chanya na athirifu kati ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu na kufichua njama za maadui wa Uislamu za kuwafarakanisha Waislamu, zilikuwa miongoni mwa ajenda muhimu zilizojadiliwa katika mkutano huo.

Duru za kisiasa katika Ulimwengu wa Kiislamu zimeuelezea mkutano wa umoja wa Kiislamu mjini Lahore kuwa ni dhihirisho safi na la kuvutia la umoja baina ya Shia na Sunni na kwamba udharura wa kuimarisha umoja huo unahisika zaidi wakati huu kuliko wakati mwingine wowote. Sasa hivi Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo utatuzi wake utawezekana kwa kuwepo umoja tu kati ya Waislamu. Sababu ni kuwa nchi za kikoloni za Magharibi zinazopigia upatu kaulimbiu ya ati kutetea haki za binadamu zinafikiria maslahi yao tu, bila kujali wala kuzithamini jamii zinginezo duniani.
Kuhusiana na maudhui hiyo, Hujjatul Islam Seyyid Ahmad Shahrokhi, mtaalamu wa masuala ya kidini anaitakidi kuwa "ili kutatua tofauti, ambazo ni kitu cha kawaida, tukizingatia hali ya kikabila na tofauti za kijiografia, inatupasa tutilie mkazo nukta ya umoja; na kwamba Mtume Muhammad SAW ndiye mhimili mkuu wa upendo na mshikamano kwa ajili ya kuwaunganisha pamoja Waislamu wa madhehebu tofauti.

Kwa hivi sasa, suala la Afghanistan na haja ya nchi hiyo kupatiwa misaada ya haraka ya kibinadamu ndilo tatizo linalohitajia utatuzi wa haraka zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu; na kwa hivyo, kutokana na kutambua hali halisi ilivyo, inapasa maulamaa wa Kiislamu, wawe wa Kishia au wa Kisuni wafanye jitihada kwa umoja na mshikamano za kusaidia kutatua tatizo hilo. Lakini mbali na Afghanistan, kadhia ya Waislamu Warohingya nchini Myanmar, ni tatizo jengine kubwa linalohitaji kushughulikiwa na Ulimwengu wa Kiislamu, lakini inasikitisha kwamba, katika miaka ya karibuni hazijafanyika jitihada za dhati za kuwasaidia na kuwaondolea masaibu yanayowapata kila uchao Waislamu hao, jambo ambalo linalifanya jukumu na masuulia ya maulamaa wa Kiislamu ya kusaidia kutatua changamoto za Ulimwengu wa Kiislamu yawe na uzito na umuhimu mkubwa zaidi.
Hujjatul Islam Gholamhossein Shahsavari, mtaalamu wa masuala ya kidini ana haya ya kunena kuhusiana na nukta hiyo:
Uislamu ni dini ya umoja, mshikamano na kuwa kitu kimoja. Wenzo na silaha kubwa zaidi ambayo maadui wa Uislamu wamekuwa wakiitumia hadi sasa ni kufarakanisha; na daima wamekuwa wakipigania kufikia malengo yao machafu na maovu kwa kuchochea mfarakano baina ya Waislamu.

Alaa kulli hal, kufanyika mkutano wa umoja wa Kiislamu mjini Lahore kunaonyesha kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu una uwezo na fursa nyingi za kutumia kuimarisha umoja; na hilo ndilo jambo linalowatia wasiwasi zaidi maadui wa Uislamu. Kujitahidi kuzima njama za matapo yanayoshupalia vitendo vya ukatili kama Uwahabi, ambalo linafikiria zaidi kuzusha mifarakano na kuwasha moto wa vita na umwagaji damu baina ya jamii za Waislamu ikiwemo Pakistan yenyewe, ni jambo ambalo, mbali na kusaidia kuimarisha umoja katika jamii za Kiislamu, litawakatisha tamaa zaidi maadui wa Uislamu wenye lengo la kutoa pigo na kuudhuru umoja wa Waislamu na wakati huohuo kuwapa moyo na matumaini zaidi Waislamu wa maeneo mbalimbali wakiwemo wa Afghanistan na Myanmar ya kuweza kutatuliwa matatizo na masaibu waliyonayo.../