Jan 04, 2022 08:01 UTC
  • Utafiti: Nusu ya watoto weusi wa UK wanaishi katika umaskini

Utafiti mpya umefichua kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya watoto wenye asili ya Afrika nchini Uingereza wanakulia katika mazingira ya uchocholea na umaskini wa kupindukia.

Utafiti huo uliofanywa na Chama cha Leba kwa kutegemea data za serikali umeonesha kuwa, kuna uwezekano maradufu kwa watoto weusi katika nchi hiyo ya Ulaya kuinukia na kuishi katika umaskini, ikilinganishwa na wenzao wa Kizungu.

Ripoti ya utafiti huo imebainisha kuwa, idadi ya watoto wenye asili ya Afrika walioko katika familia za kimaskini imeongezeka maradufu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita katika nchi hiyo ya Ulaya, yaani kutoka asilimia 42 baina ya mwaka 2010-11, hadi asilimia 53 baina ya mwaka 2019-20.

Chama cha Leba kimesema hali hii ya kukatisha tamaa imetokana na utepetevu wa chama tawala cha Kihafidhina, na mwenendo wa kukana ubaguzi huu wa kimfumo.

Umaskini miongoni mwa watoto wadogo umekithiri kutokana na janga la Corona

Anneliese Dodds, Waziri Kivuli wa Masuala ya Wanawake na Usawa wa Uingereza amesema chama cha Conservative kinapaswa kuona fedheha kutokana na utendaji wake mbaya unaosababisha ubaguzi huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mfuko wa Watoto wa  Umoja wa Mataifa na shirika la Save the Children, idadi ya watoto wanaoishi katika umaskini wa namna mbalimbali imeongezeka hadi takriban bilioni 1.2 kutokana na janga la COVID-19.

Tags