Mazungumzo ya simu ya Marais wa Iran na Russia
(last modified Sun, 27 Feb 2022 03:52:12 GMT )
Feb 27, 2022 03:52 UTC
  • Mazungumzo ya simu ya Marais wa Iran na Russia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, na Rais wa Russia, Vladimir Putin, walifanya mazungumza ya simu Alhamisi iliyopita kuhusu masuala ya kimataifa na mazungumzo yanayoendelea huko Vienna kuhusu suala la kuondolewa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran.

Rais Ebrahim Raisi ameashiria mgogoro wa Ukraine na kusema: "Upanuzi wa Shirika la NATO upande wa Mashariki unaibua mivutano" na kuongeza kuwa: "Kupanuka kwa NATO ni tishio kubwa kwa utulivu na usalama wa nchi huru katika kanda mbalimbali za dunia. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ana matumaini kwamba yale yanayojiri sasa yatamalizika kwa maslahi ya mataifa ya kanda hiyo."

Kwa upande wake Rais Vladimir Putin wa Russia ameitaja hali ya sasa ya Ukraine kuwa ni jibu halali kwa miongo kadhaa ya ukiukaji wa mikataba ya usalama na juhudi za nchi za Magharibi za kuhujumu usalama wa Russia.

Suala la Ukraine na matukio yake hususan mashambulizi ya kijeshi ya Russia nchini humo limeibua majibu ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya unatathminiwa katika mkondo huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ameandika ujumbe katika mtandao wa Twitter kuhusu msimamo wa Tehran mkabala wa mashambulizi ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine akisema: Chanzo cha mgogoro wa Ukraine ni hatua za kichochezi za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO). Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza katika ujumbe huo kwamba, kutumia vita hakuwezi kuwa suluhisho. Amesema kuna udharura wa kusitishwa vita na kujikita katika juhudi za kutafuta suluhisho la kisiasa na kidemokrasia la mgogoro huo. 

Mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine

Kwa upande mwingine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran,  Saeed Khatibzadeh, ameelezea masikitiko yake juu ya kuanza kwa hatua za kijeshi na kuongezeka mzozo huko Ukraine na kusema: Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia kwa wasiwasi mkubwa yanayojiri huko Ukraine. Amesema inasikitisha kwamba kuendelea kwa chokochoko za NATO zinazoongozwa na Marekani kumesababisha hali ambayo imeliweka eneo la Eurasia kwenye hatihati ya kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazitaka pande husika kusitisha uhasama na kusimamisha mapigano kwa ajili ya mazungumzo ya haraka ya kutafutasuluhisho la kisiasa la mgogoro huo. Vilevile amesisitiza haja ya kuheshimiwa sheria za kimataifa na za haki za kibinadamu katika mizozo ya kijeshi. 

Msimamo wa Iran kuhusu mgogoro wa Ukraine na mashambulizi ya Russia dhidi ya nchi hiyo unawiana na misimamo jumla ya Tehran ya kukosoa mchango hasi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na shirika la NATO duniani hasahasa huko Ulaya na Asia Magharibi. Marekani, kama kinara wa NATO, siku zote imekuwa ikitoa wito wa kuwepo sera na hatua za kichokozi na kupanuliwa Shirika la Kijeshi za Nchi za Magharibi (NATO) upande wa Mashariki kwa lengo la kuidhibiti Russia, kuidhoofisha na hatimaye kuisambaratisha kabisa. Msimamo huo wa uhasama wa NATO unaoongozwa na Marekani awali ulikabiliwa na maonyo ya mara kwa mara kutoka Moscow kuhusu haja ya kubadilishwa mtazamo huo. Russia ilifanya jitihada kubwa na hata kutoa mapendekezo ya kiusalama kwa nchi za Magharibi. Hatimaye na baada ya Washington na NATO kukataa kutoa jibu chanya kwa matakwa ya kiusalama ya Moscow, na kushikamana Ukraine na NATO katika jitihada za jumuiya hiyo ya kijeshi za kuiburuta Kiev upande wake, Russia imechagua suluhisho la kijeshi ambalo limesababisha mzozo wa sasa. Serikali ya Ukraine ndiyo iliyotayarisha mazingira ya hali mbaya ya sasa nchini humo kwa kuhadaika na ahadi za Magharibi hasa suala la kuingia nchi hiyo katika kambi ya Magharibi na kujiunga na shirika la NATO, ambao ni mstari mwekundu kwa usalama wa Russia.

Wakati huo huo nchi za Magharibi ambazo ziliahidi kuitetea Kiev, sasa zimeiacha peke yake na kutosheka tu kwa kuiwekea Russia baadhi ya vikwazo. Katika upande mwingine Moscow imetangaza kuwa iko tayari kulipa gharama yoyote kwa sababu inaliona suala la upanuzi wa NATO kuelekea Mashariki kuwa suala la kuwepo au kuangamia kwa Russia.

Mashambulio makali ya Russia ndani ta Ukraine

Javad Vaidi, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa, anasema: “Sababu ya stratijia ya Vladimir Putin ya kutekeleza operesheni ya kijeshi nchini Ukraine ni kuhakikisha usalama na kulinda uhai wa Russia mpya, kwani iwapo Russia itashindwa tena kwa sababu yoyote ile, hatua inayofuata itakuwa kusambaratika Shirikisho la Russia na kushika mamlaka wanasiasa wenye mielekeo ya Kimagharibi huko Moscow.”

Pamoja na hayo yote, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa wito wa kusitishwa vita na kutatuliwa mzozo wa Ukraine kwa njia ya mazungumzo na utatuzi wa kisiasa. Msimamo huu pia umekaribishwa na maafisa wa serikali ya Ukraine. Akijibu ujumbe wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian, balozi wa Ukraine mjini Tehran, Sergey Burdylyak amesema: "Vita kamwe haviwezi kuwa suluhisho sahihi kwa tatizo lolote. Nakubaliana na Mheshimiwa Amir Abdollahian.”