Borell apendekeza China iwe mpatanishi kati ya Russia na Ukraine
(last modified Sun, 06 Mar 2022 04:22:39 GMT )
Mar 06, 2022 04:22 UTC
  • Borell apendekeza China iwe mpatanishi kati ya Russia na Ukraine

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amependekeza nchi ya tatu iwe mpatanishi wa kumaliza mivutano kati ya Russia na Ukraine.

Josep Borrell, ametaka China iwe mpatanishi  baina ya Russia na Ukraine ili kuhitimisha vita vinavyoendelea kati ya nchi hizo mbili.

Hakuna maelezo na ufafanuzi zaidi uliotolewa kuhusu wito huo na pendekezo hilo lililotolewa na mkuu huyo wa sera za nje wa EU.

Siku ya Ijumaa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin alizitolea mwito pande zinazopigana nchini Ukraine kuwa na stahamala, kutochukua hatua za kushadidisha mivutano na kudhamini usalama wa vituo vya nchi hiyo vinavyohusiana na masuala ya nyuklia.

Rais Vladimiri Putin wa Russia (kulia) na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine

Sambamba na vita vya Ukraine kuingia katika siku ya 11, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR amesema, hadi sasa zaidi ya watu milioni moja na laki mbili wamevuka mipaka na kuihama Ukraine na akatahadharisha kuwa mgogoro wa wakimbizi wa nchi hiyo ndio kwanza umeanza.

Halikadhalika, wakati vita na mapigano yanaendelea nchini Ukraine, idadi kadhaa ya raia wa Russia nao pia wanaihama nchi yao na kuelekea Finland kutokana na athari hasi za vita hivyo pamoja na sera mpya zilizotangazwa na serikali ya Moscow.../

Tags