Upinzani dhidi ya uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya
(last modified Tue, 08 Mar 2022 11:30:03 GMT )
Mar 08, 2022 11:30 UTC
  • Upinzani dhidi ya uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya

Mjumbe mmoja wa ngazi za juu katika bunge la Ujerumani amesema kuwa mkondo wa kuipa Ukraine uanachama katika Umoja wa Ulaya ni hatari kwa maslahi ya umoja huo na kwamba njia bora ni kuipa Ukraine uanachama wa heshima tu.

Akifafanua suala hilo, Michael Roth, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Ujerumani, amesema katika mahojiano kwamba: "Kinachoweza kutegemewa na uongozi wa Ukraine ni uanachama wa heshima tu katika Umoja wa Ulaya, na uzoefu wa huko nyuma wa Umoja wa Ulaya kujipanua katika nchi za Balkan ulishuhudia makosa yakifanyika katika uwanja huo." Kuhusu ugumu wa mchakato wa kupewa uanachama katika Umoja wa Ulaya, amesema: "Ili kujiunga na EU, ni muhimu kwamba nchi ziwe na nguvu za kiuchumi na thabiti na ziwe na usimamizi mzuri katika kupambana na ufisadi. Kwa upande mwingine, kurasa 50,000 za sheria za EU zinapaswa kutafsiriwa katika sheria za kitaifa za Ukraine. Hili ni suala muhimu na halitatokea mara moja."

Rais Volodymyr Zelinsky wa Ukraine ametaka nchi hiyo iruhusiwe kujiunga na Umoja wa Ulaya kufuatia mashambulio ya Russia nchini humo, akisisitiza kwamba kuthibitishwa uanachama wa Ukraine katika umoja huo kutaonyesha uungaji mkono wake kwa Kiev.

Michael Roth

Kuhusu suala hilo Petro Poroshenko, rais wa zamani wa Ukraine amesema: "Kujiunga Ukraine na Umoja wa Ulaya na NATO ni lengo la kimkakati kwetu,"

Pamoja na hayo lakini upinzani nchini Ujerumani, nchi muhimu na yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, dhidi ya uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya umekatiza matumaini ya rais wa nchi hiyo ya kuwa mwanachama wa haraka katika umoja huo, na kwa sasa hakuna mtazamo wowote chanya kwa Ukraine kuhusu suala hilo.

Msimamo huo wa Berlin, bila shaka umeungwa mkono pia na afisa mkuu mtendaji wa Umoja wa Ulaya. Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesema mchakato wa kujibu ombi la Ukraine la kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya bila shaka ni jambo litakalochukua muda mrefu. Amesema licha ya kuwa watu wa Ukraine ni wa familia ya Ulaya, lakini uanachama wa EU una mchakato wa kupitia, na hayo ni baada ya Bunge la Ulaya kuidhinisha ombi la Ukraine kupewa uanachama katika umoja huo Jumanne iliyopita.

Bila shaka, linapokuja suala la kupewa uanachama katika Umoja wa Ulaya, huo huwa ni mchakato mrefu na ngumu sana unaohitaji kukamilishwa masharti mengi ambayo huchukua miaka kadhaa kukamilika. Uturuki, kwa mfano, imekuwa katika harakati za kujiunga na Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2005, na baada ya miaka mingi ya kujaribu kufikia lengo hilo haijafikia popote na hilo ni kutokana na upinzani mkali na kutotimizwa masharti ya Brussels.

Kwa upande wa Ukraine pia, kwa kuzingatia vipimo na viwango vya Umoja wa Ulaya na kuwa mbali nchi hiyo na viwango hivyo, na hasa kuhusiana na suala zima la kupambana na rushwa na ufisadi wa kiutawala, ombi la Rais Zelinsky la kutaka Ukraine ijiunge na EU mara moja halitawezekana. Ukraine sasa inashikilia nafasi ya 117 katika masuala ya kuenea rushwa duniani na ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa rushwa barani Ulaya. Hali ya kiuchumi ya Ukraine pia imekuwa ikidorora katika miaka ya hivi karibuni.

Rais Volodymyr Zelinsky wa Ukraine

Hayo yote yameifanya nchi hiyo kupoteza fursa ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Wakati huo huo, moja ya masharti muhimu zaidi ambayo Umoja wa Ulaya umeyaweka kwa ajili ya nchi zinazotaka kupewa uanachama katika umoja huo, ni utatuzi wa migogoro ya kieneo na mipaka na majirani zao. Muhimu zaidi, Ujerumani ambayo ni moja ya wanachama wakuu wa Umoja wa Ulaya, haitaki kupoteza nafasi yake hiyo ya juu mkabala na uanachama wa nchi kubwa kama Ukraine, ambayo ni nchi kubwa zaidi barani Ulaya kimasafa na yenye idadi kubwa ya watu. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, uanachama wa Ukraine utapunguza kwa kiwango fulani nguvu ya kupiga kura ya Ujerumani katika taasisi za Ulaya na hivyo kupunguza ushawishi wake barani humo.

Tags