Safari ya Johnson Saudi Arabia; mafuta mhimili wa mazungumzo
(last modified Wed, 16 Mar 2022 07:15:05 GMT )
Mar 16, 2022 07:15 UTC
  • Safari ya Johnson Saudi Arabia; mafuta mhimili wa mazungumzo

Wakati vita vya Russia na Ukraine vikiendelea na bei ya mafuta duniani kuendelea kupanda pia, Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza anaelekea Saudi Arabia kwa ajili ya kujadili suala la kupewa mafuta kwa bei rahisi.

Safari hiyo inafanyika huku bei ya mafuta katika vituo vya mafuta ikifikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma ambapo kwa sasa lita moja ya petroli inauzwa kwa pauni 1.60 huku dizeli ikiuzwa kwa pauni 1.70 nchini Uingereza. Sajid Javid, Waziri wa Afya wa Uingereza  amesema Johnson anahitaji kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo kwa sababu wanahitaji mafuta ya bei nafuu kufuatia uvamizi wa Russia nchini Ukraine.

Hivi karibuni, bei ya mafuta imefikia kiwango cha juu zaidi katika miaka 14 iliyopita, ambao pipa moja la mafuta ya Brent limeuzwa kwa karibu dola 140. Pia, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, bei ya mafuta katika masoko ya dunia imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60, ambapo bei ya bidhaa nyingine pia imeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Ziara ya Johnson nchini Saudi Arabia inakuja wakati nchi hiyo hivi majuzi iliwanyonga kwa umati watu 81 wakiwemo Wayemen saba na Msyria mmoja, kwa tuhuma bandia za kuhusika na ugaidi na uhalifu mwingine, ikiwa ni pamoja na kuwa na "imani potofu," katika mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutekelezwa katika miongo kadhaa iliyopita. Jinai ya kuwanyonga kwa umati wahanga hao imetekelezwa dhidi ya vijana ambao walitumia haki yao halali ya kutoa maoni, na hivyo kuibua hisia na hasira za wanaharakati wengi wa kimataifa wa haki za binadamu.

Boris Johnson

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Michel Bachelet, amelaani jinai ya kunyongwa watu 81 nchini Saudi Arabia, na kuzitaja kesi zilizoendeshwa dhidi yao kuwa zisizo za haki, akisema: "Hukumu ya kifo ilitolewa dhidi yao wakati masharti ya kesi hayakutekelezwa ipaswavyo, na baadhi ya walionyongwa hata hawakuweza kupata hakikisho la kupata hukumu ya kiadilifu.

Kwa hakika, Uingereza na Marekani na washirika wao wa Ulaya, licha ya kauli mbiu zote wanazotoa eti za kutetea haki za binadamu, lakini hivi sasa wakati ambapo Saudi Arabia inakiuka wazi haki za binadamu, si tu kwamba hawalaani jinai hiyo, bali wanafanya juhudi za kuimarisha ushirikiano na nchi hiyo ya Kiarabu. Kuhusiana na hilo, Waziri wa Afya wa Uingereza amekiri kwamba London inafahamu vyema ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia, lakini pamoja na hayo ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.

Makadirio yanaonyesha kuwa Saudi Arabia ina uwezo wa ziada wa kuzalisha mapipa milioni mbili kwa siku, na kwamba nchi za Magharibi zinakusudia kuitumia nchi hiyo kama silahakatika vita vyao vya kiuchumi na Russia.

Nchi za Magharibi katika migogoro kama vile ya vita vya Yemen na mauaji ya Jamal Khashoggi pia zilionyesha kuwa zinazingatia maslahi yao tu na kwamba kuheshimu haki za binadamu si chochote zaidi ya kauli mbiu kwao. Ni kwa msingi huo ndio maana nchi kama vile Uingereza na washirika wake hazijasimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni kuhusu vita vya Yemen, bali zimeamua kupanua uhusiano wao na Saudi Arabia.

Ned Price

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Ned Price pia amekataa kulaani hukumu ya kifo iliyotekelezwa na Saudi Arabia dhidiya raia wasio na hatia ikiwa ni katika kuendeleza siasa za undumakuwili za Washington katika ngazi za kimataifa, licha ya kwamba utawala wa Biden umekuwa ukidai kutoa kipaumbele kwa suala la haki za binadamu.

Utabiri uliopo ni kwamba iwapo Russia itaendeleza vita huko Ukraine na kuendelea kususiwa kimataifa mafuta na gesi yake, nchi zinazozalisha mafuta na gesi hazitaweza kufidia kwa haraka upungufu uliopo sokoni, na hivyo kuongeza uwezekano wa bei ya mafuta duniani kufikia dola 200 kwa pipa. Kwa hivyo ni wazi kuwa, kwa sasa nchi za Magharibi zimeamua kulinda maslahi yao na kudhibiti bei ya mafuta kwa kupuuza jinai zote za Saudi Arabia dhidi ya raia wake yenyewe na wengine wa kigeni.