CNN: Wamarekani wengi wanaona US inaelekea kusiko
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika hivi karibuni yanaonesha kuwa, aghalabu ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa, taifa lao lipo katika mkondo usio sahihi.
Televisheni ya CNN ya Marekani imenukuu matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Monmouth yanayoonesha kuwa, asilimia 73 ya Wamarekani waliohojiwa wanaitakidi kuwa nchi yao inaelekea kusiko.
Ripoti hiyo imeeleza bayana kuwa, robo tatu ya watu waliohojiwa kwenye utafiti huo walitumia maneno hasi kuhusu hali ya hivi sasa ya Marekani.
Watafiti wa uchunguzi huo wa maoni waliwataka waliohojiwa kuieleza Marekani kwa neno moja, na neno lililotumika zaidi ni 'mgawanyiko' na maneno yanayoshabihiana na neno hilo kama mpasuko, mparaganyiko na mzozano.
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa na shirika la Axios-Ipsos mwaka jana ulionesha kuwa, asilimia 80 ya Wamarekani wote wanaamini kuwa nchi yao inaelekea kusambaratika.
Tafiti za huko nyuma zimewahi kufichua kuwa, Wamarekani ni miongoni mwa watu wanaonung'unika na kulalamika zaidi duniani.