Zemmour: Nitawafukuza wahajiri wa Afrika nikichaguliwa kuwa rais wa Ufaransa
Mgombea mwenye siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa rais wa Ufaransa, Éric Zemmour amesema atawafukuza malaki ya wahamiaji wa Kiafrika, iwapo atachaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo ya Ulaya mwezi ujao.
Éric Zemmour anayejulikana kwa mitazamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu na wahamiaji amesema, iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Ufaransa, basi atabuni wizara maalumu itakayotwikwa jukumu la kuwatimua nchini humo mamia ya maelfu ya wahajiri ndani ya muhula wake wa kwanza wa miaka mitano.
Kadhalika mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa Ufaransa amedai kuwa, atazuia mali na fedha za viongozi wa Kiafrika zilizoko nchini humo, iwapo viongozi hao watakataa kuwapokea raia wa nchi zao walioko Ufaransa.
Zemmour amesema akichaguliwa kuwa rais, ataenda Algeria, Morocco na Tunisia kuzungumza na viongozi wa nchi hizo juu ya suala la kuwafukuza raia wa nchi hizo wanaoishi Ufaransa. Asilimia 30 ya wahajiri walioko Ufaransa wanatoka katika nchi hizo tatu za kaskazini mwa Afrika.
Mbali na kuwa na chuki na misimamo hasi dhidi ya wahajiri, mwanasiasa huyo amekuwa akitangaza wazi wazi chuki zake dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mapema mwaka huu, alisema ajenda na mipango yake kuhusu dini ya Kiislamu inajumuisha marufuku ya uvaaji wa nguo zote zenye alama za Kiislamu - ikiwa ni pamoja na vazi la hijabu - katika viwanja vya umma, pamoja na marufuku ya kujenga minara na misikiti nchini Ufaransa.
Alisema kuwa atawazuia Waislamu nchini Ufaransa kuwapa watoto wao jina la "Muhammad" endapo atashinda kiti cha Rais wa Jamhuri, na kuongeza kuwa ataweka jedwali la majina wanayopewa watoto wa Kiislamu.