Ukraine iko tayari kubadili Katiba na kutupilia mbali kujiunga na NATO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81978-ukraine_iko_tayari_kubadili_katiba_na_kutupilia_mbali_kujiunga_na_nato
Waziri Mkuu wa Slovenia ametangaza utayarifu wa Ukraine wa kubadilisha Katiba ya nchi hiyo na kuachana na nia yake ya kujiunga na NATO.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 31, 2022 07:58 UTC
  • Waziri Mkuu wa Slovenia, Janez Janša
    Waziri Mkuu wa Slovenia, Janez Janša

Waziri Mkuu wa Slovenia ametangaza utayarifu wa Ukraine wa kubadilisha Katiba ya nchi hiyo na kuachana na nia yake ya kujiunga na NATO.

Hayo yameelezwa huku operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine ikiingia siku yake ya 36. Russia iliishambulia Ukraine baada ya nchi hiyo na washirika wake wa Magharibi kuendeleza sera zao za kupanua Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) upande wa Mashariki hadi kwenye mipaka ya Russia. 

 Waziri Mkuu wa Slovenia, Janez Janša amesema kuwa maafisa wa Ukraine wametaka kupata dhamana rasmi na madhubuti ili kuhakikisha usalama wao.

Janša amebainisha kuwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelinsky, Waziri Mkuu wa Ukraine Denis Schmihal na maafisa wenzake, wamesema kuwa baada ya yaliyojiri nchini humo, Ukraine iko tayari kubadilisha katiba ya nchi, kutupilia mbali nia ya kujiunga na NATO na kuwasilisha katiba iliyopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Slovenia, Waukraine wanataka dhamana rasmi ya usalama wao na wanaamini kwamba dhamana rasmi itapatikana kwa kupewa uanachama wa kudumu katika Umoja wa Ulaya.