Maambukizi ya UVIKO-19 yaongezeka Uingereza
Idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa UVIKO1-19 nchini Uingereza khususan wale wanaopatwa na maambukizi aina mpya ya kirusi cha corona cha Omicron inazidi kuongezeka.
Takwimu zinaonyesha kuwa, hadi sasa zaidi ya watu milioni 21 na 410,000 wameambukizwa UVIKO-19 huko Uingereza na 166,000 wameaga dunia kwa ugonjwa huo. Shirika la habari la IRNA leo limeripoti kuwa, katika hali ambayo maambukizi ya corona nchini Uingereza yalikuwa yakipanda na kushuka miongoni mwa makundi ya watu wenye umri wa chini; hivi sasa kwa mara nyingine tena maambukizi ya ugonjwa huo yameripotiwa kuongezeka miongoni mwa wazee wanaougua maradhi mengineyo.
Takwimu zilizotolewa na Chuo cha Imperial cha London zinaonyesha kuwa, aina mbili za maambukizi ya kirusi cha corona cha Omicroni yaani BA. na BA.2 ambavyo vimetambuliwa kama aina kuu ya virusi vya corona vilisababisha ongezeko kubwa la corona mwezi Januari na Machi huko Uingereza. Matokeo ya sampuli za wagonjwa zilizochukuliwa kuanzia Machi 8 hadi 31 mwaka huu zinaonyesha kuwa asilimia 6.37 ya wananchi wa Uingereza waliambukizwa UVIKO-19; kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kusajiliwa tangu dunia kukumbwa na corona mwezi Disemba mwaka 2019.

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu Uingereza kwa upande mmoja ilishuhudia kupungua maambukizi ya corona miongoni mwa watu wenye umri wa kuanzia miakak 5 hadi 17 na 18 hadi 55; na katika upande mwingine maambukizi ya UVIKO-19 yaliongezeka kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55.