Shehbaz Sharif achaguliwa kuwa Waziri Mkuu Pakistan baada ya Khan kutimuliwa
(last modified Tue, 12 Apr 2022 02:29:52 GMT )
Apr 12, 2022 02:29 UTC
  • Shehbaz Sharif achaguliwa kuwa Waziri Mkuu Pakistan baada ya Khan kutimuliwa

Bunge la Pakistani limemchagua Shehbaz Sharif kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya mtangulizi wake, Imran Khan, kuondolewa na wabunge wengi wa chama chake kujiuzulu kutoka katika Bunge la Kitaifa.

Siku ya Jumatatu na kufuatia mzozo wa kikatiba wa wiki nzima ambao ulipelekea kupigwa kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Khan, wabunge wa Pakistani wamemchagua Shehbaz Sharif mwenye umri wa miaka 70, kuwa waziri mkuu.

Sharif ni kaka mdogo wa Nawaz Sharif, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa mihula mitatu isiyofuatana na hatimaye kuondolewa madarakani na Mahakama ya Juu ya Pakistan mwaka 2017.

Shehbaz aliibuka kuwa kiongozi wa upinzani ulioungana wa kumng'oa Khan madarakani, ambaye amesema serikali yake imeangushwa  katika njama iliyopangwa na Marekani.

Muda mfupi kabla ya upigaji kura kuanza siku ya Jumatatu, wabunge kutoka chama cha Khan - Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) – walijiuzulu kwa wingi kutoka Bunge la Chini ili kuelezea upinzani wao dhidi ya serikali tarajiwa.

Imran Khan 

Tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1947, hakuna waziri mkuu wa Pakistan ambaye amemaliza muhula wake kamili. Hata hivyo, Khan ndiye wa kwanza kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Huku Khan akiendelea kupinga hatua ya kumuuzulu, maelfu ya Wapakistan katika miji kadhaa walifanya maandamano kupinga kuondolewa kwake madarakani.