Mafuriko na maporomoko ya ardhi yaua watu 58 nchini Ufilipino.
Watu karibu 60 wameaga dunia kutokana na kimbunga kilichosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Ufilipino.
Shirika la habari la Associated Press limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Kimbunga cha Tropiki cha Megi kimesababisha nchi hiyo kushuhudia mvua kubwa, mafuriko na maporoko ya udongo hususan katika mkoa wa kati wa Leyte.
Habari zinasema kuwa, mbali na watu 58 kuaga dunia na mamia ya wengine kujeruhiwa, maelfu wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi.
Watu 47 wameripotiwa kuaga dunia baada ya maporomoko ya ardhi kusomba vijiji 6 katika jiji la Baybay, huku wengine 27 wakitoweka. Kufuatia hali hiyo serikali na wananchi wa Ufilipino wameomba misaada ya dharura hasa ya chakula.
Watu wengine watatu wameaga dunia katika mkoa wa kati wa Negros Oriental, na wengine watatu katika kisiwa cha Mindanao, kilichoko kusini mwa nchi hiyo kusini mashariki mwa Asia.

Disemba mwaka jana 2021, watu wasiopungua 375 walipoteza maisha katika mafuriko mengine yaliyosababishwa na mvua kubwa huko Ufilipino.
Aidha mwaka 2013, kimbunga kikali cha Haiyan kiliua zaidi ya watu elfu 8 huko Uflipino, nchi ambayo inashuhudia vimbunga zaidi ya 20 kila mwaka.