Wanafunzi Waislamu Marekani wahanga wa vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji mashuleni
Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya wanafunzi Waislamu katika skuli za jimbo la California nchini Marekani wanakabiliwa na vitendo vya ubaguzi wanavyofanyiwa na wanafunzi wakubwa kwa wadogo wakiwemo walimu.
Shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, zaidi ya nusu ya wanafunzi Waislamu katika sule za jimbo la Califiornia ambao ni sawa na asilimia 55.73 wamesema katika uchunguzi wa maoni uliofanywa na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) kwamba, wamekuwa wakijisikia kutokuwa salama, kutokubalika au kukosa furaha wanapokuwa mashuleni kutokana na utambulisho wao wa Kiislamu.
Kiwango hicho ni cha juu kuwahi kuripotikwa tangu Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) lianze kufanya uchunguzi wa maoni kama huu mwaka 2013. Wakati huo huo mahojiano waliyofanyiwa wanafunzi Waislamu katika shule za jimbo la California yanaonyesha uwepo wa kiwango cha juu sana cha vitendo vya uonevu, kunyanyaswa na kubaguliwa na wanafunzi wenzao wa rika lao, wakubwa kuliko wao na hata walimu wao.
Ripoti iliyoandaliwa na CAIR mwaka jana wa 2021 inaonyesha kuwa, takriban nusu ya wanafunzi Waislamu huko California ambao ni asilimia 47.1 walieleza kuwa, wanakabaliwa na hujuma za unyanyasaji na kudhalilishwa kutokana na kuwa kwao Waislamu. Kiwango hocho cha unyanyasaji kimetajwa kuwa mara mbili ikilinganishwa na kile cha wastani wa asilimia 20 kilichoripotiwa hapo kabla.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kwamba takriban thuluthi moja ya wanafunzi Waislamu katika shule za California wamepitia au kushuhudia aina fulani ya unyanyasaji wa mtandaoni.
Hapo awali, uchunguzi uliofanywa nchini Marekani uligundua kuwa zaidi ya nusu ya Waislamu nchini humo wanakumbwa na hujuma na mashambulizi dhidi ya Uislamu angalau mara moja katika maisha yao.