Russia yakosoa juhudi za Magharibi za kurefusha vita vya Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82758-russia_yakosoa_juhudi_za_magharibi_za_kurefusha_vita_vya_ukraine
Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu amesema kwamba Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimefanya jitihada kubwa za kurefusha muda wa operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2022 04:41 UTC
  • Jenerali Sergei Shoigu
    Jenerali Sergei Shoigu

Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu amesema kwamba Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimefanya jitihada kubwa za kurefusha muda wa operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine.

Jenerali Sergei Shoigu amesema, hatua ya nchi za Magharibi ya kuendelea kutuma silaha nchini Ukraine inaonyesha wazi nia ya nchi hizo ya kuendelea kuisukuma nchi hiyo katika mapigano na vita hadi pale mwanajeshi wa mwisho wa Ukraine atakapoangamizwa.

Ukosoaji wa afisa huyo mkuu wa kijeshi wa Russia kuhusu mwenendo wa nchi za Magharibi katika vita vya Ukraine una mantiki, hasa kutokana na juhudi zinazoongozwa na Marekani za kuendelea kutuma kiasi kikubwa cha zana na silaha mbalimbali za kivita nchini humo. Nukta muhimu ni kuwa, kiwango na aina ya silaha hizo, taratibu, zinaelekea kwenye silaha kubwa kama vile ndege na helikopta za kivita, magari ya kijeshi ya deraya, mifumo ya ulinzi wa anga na kadhalika.

Katika mkondo huo jarida la Wall Street Journal limeripoti kwamba, Pentagon na kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza zana za kijeshi ya nchi hiyo, Lockheed Martin, walikuwa kwenye mazungumzo ya kuongeza uzalishaji wa silaha kwa ajili ya Ukraine.

Wakati huo huo, Jenerali Mark Milley, mkuu wa vikosi vya majeshi ya Marekani, siku ya Jumanne iliyopita, akihutubia mkutano wa maafisa wa kijeshi kutoka nchi 13 washirika wa Washington, alitoa wito wa kuharakishwa msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Msemaji wa mkutano huo, Dave Butler, alisema: "Viongozi wa kijeshi wa nchi zilizoshiriki wametathmini na kubadilishana maoni juu ya hujuma ya Russia huko Ukraine, ikiwa ni pamoja na misaada ya aina mbalimbali kwa Kiev ili kurejesha na kutetea mamlaka yake."

Marekani inazidisha utumaji wa silaha nchini Ukraine

Katika mkutano wa siku ya Jumanne pia viongozi wa nchi za Magharibi walisisitiza makubaliano yao juu ya haja ya kuongeza shinikizo kwa Russia, ikiwa ni pamoja na kuweka vikwazo zaidi na kuendelea kuitenga Moscow kimataifa.

Ni wazi kwamba, Marekani na washirika wake wa Ulaya na wasio wa Ulaya, kama vile Canada, Australia na hata Japan, wanaviona vita vya Ukraine kuwa ni fursa ya kipekee kwa ajili ya kulipiza kisasi dhidi ya Rassia na kiongozi wa nchi hiyo, Vladimir Putin ambaye kwa kipindi chote cha miongo miwili, amesimama kidete mkabala wa sera za kibabe na za kupenda makuu za Marekani na NATO huko Ulaya, Asia Magharibi, Amerika Kusini na hata Kaskazini. Hii ni pamoja na kuwa, katika maoni ya viongozi wa nchi za Magharibi, ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine na karibu na maeneo jirani na NATO, utakuwa na maana ya kudharaulika na kupoteza heshima shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi na kupanuka zaidi ushawishi na nguvu za kikanda na kimataifa za Russia; suala ambalo litabadili mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya kwa maslahi ya Russia. Kwa hivyo, nchi hizo zimeazimia haswa kuzuia ushindi wa Russia kwa gharama yoyote. Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alisisitiza Jumanne iliyopita kwamba, wanajeshi wa Russia hawapaswi kuruhusiwa kupata ushindi katika vita vya Ukraine. Scholtz alisema: "Sisi sote katika Umoja wa Ulaya na washirika wetu tunaamini kikamilifu kwamba, Russia haipasi kushinda vita hivi."

Olaf Scholz

Kwa kuzingatia azma ya Russia ya kushinda vita vya Ukraine na vilevile mabadiliko ya mbinu yake ya kijeshi ya kijielekeza zaidi kwenye operesheni za kijeshi Mashariki mwa Ukraine kwa shabaha ya kulifurusha jeshi la nchi hiyo katika maeneo yote ya mikoa miwili ya Donetsk na Luhansk na kuifanya nchi mbili huru na zinazojitawala, inatazamiwa kuwa Marekani na washirika wake watazidisha maradufu misaada yao ya kijeshi kwa Ukraine katika siku za usoni. Lengo la nchi za Magharibi ni kuimarisha uwezo wa jeshi la Ukraine na makundi ya wanamgambo wa nchi hiyo ili kukabiliana na Russia, na hivyo kuzidisha hasara za kinafsi za wanajeshi na uharibifu wa silaha, na hatimaye kuilazimisha Moscow kusimamisha operesheni za kijeshi, hasa huko Mashariki mwa Ukraine.

Hata hivyo maafisa wa Russia wanasisitiza kwamba wataendeleza hatua za kijeshi katika eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov amesema: "Awamu nyingine ya operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine kwa ajili ya kukomboa Jamhuri za watu wa Donetsk na Luhansk imeanza, na nina uhakika kwamba hiki kitakuwa kipindi muhimu sana katika operesheni hii maalumu."