May 04, 2022 02:33 UTC
  • Mivutano inayoongezeka katika uhusiano kati ya Russia na utawala wa Kizayuni wa Israel

Uhusiano kati ya Russia na utawala wa Kizayuni wa Israel umeingia katika kipindi kipya na cha wasiwasi na mivutano baada ya kuanza mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine kutokana na misimamo ya Tel Aviv ya kuwa pamoja na nchi za Magharibi na kuchukua misimamo dhidi ya Russia.

Katika uwanja huo, matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov yamezusha utata mpya katika uhusiano kati ya Moscow na Tel Aviv na kuibua misimamo mikali ya maafisa wa Kizayuni. Katika mahojiano yake na televisheni ya Italia, Lavrov amejibu swali kwamba, inakuwaje Russia inadai kuwa inataka kuangamiza kabisa Unazi nchini Ukraine ilhali Rais wa nchi hiyo mwenyewe, Volodymyr Zelenskyy ni Myahudi? Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: "Hoja ya Zelenskyy ni kwamba 'Unazi unawezaje kuwepo Ukraine wakati yeye ni Myahudi?' Yumkini nikakosea, lakini ninavyoelewa mimi Adolph Hitler pia alikuwa na damu ya Kiyahudi."  

Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett ameyataja matamshi hayo ya Lavrov aliyesema kwamba Hitler alikuwa Myahudi kuwa ni "hatari sana", kinyume na ukweli za yasiyokubalika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid pia amemkosoa vikali mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov kwa matamshi hayo yaliyosema kuwa Hitler alikuwa na damu ya Kiyahudi kwenye mwili wake. Lapid amesema, matamshi ya Lavrov hayasameheki na ni ya kuaibisha. Viongozi wengine wa Kizayuni na wa jamii ya Kiyahudi pia wamemkosoa vikali Lavrov.

Yair Lapid

Inaonekana kuwa matamshi hayo ya Lavrov yametolewa kwa lengo la  kulalamika na wakati huo huo ni onyo la Moscow kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao hatua kwa hatua unabadilisha msimamo wake wa awali wa kutoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine na kujiunga na kambi ya Magharibi na hata kutangaza utayarifu wake wa kutuma msaada wa silaha nchini Ukraine; suala ambalo linaonesha waziwazi msimamo wa chuki dhidi ya Russia.

Maafisa wa Israel wanadai kuwa, hapo awali walitoa vifaa vya usalama kwa Ukraine lakini hivi karibuni hawajatoa silaha kwa nchi hiyo. Hata hivyo, ushahidi unathibitisha kwamba, Tel Aviv imefanya kile kinachoitwa chaguo la kihistoria na kuegemea upande wa Magharibi dhidi ya Russia, kwa kuzingatia matukio ya miezi ya hivi karibuni na kushadidi hatua za kambi ya Magharibi zinazoongozwa na Marekani dhidi ya Russia. Suala hilo limedhihirika waziwazi hasa katika msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid, ambaye ameituhumu Russia kuwa imefanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Msimamo wa Lapid hususan katika suala hili nyeti sana, yaani kuishutumu Russa kuwa imefanya jinai ya kivita nchini Ukraine, kwa hakika umesababisha mvutano na mdororo usio na kifani katika uhusiano wa Moscow na Tel Aviv; na hapana shaka kuwa msimamo wa hivi karibuni wa Lavrov ni jibu la Moscow kwa tuhuma hizo za Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel.

Kubadilika kwa msimamo wa Israel kuhusu vita vya Ukraine kumetoa dhoruba kubwa sana kwa Russia, ambayo daima imekuwa ikidhani kuwa ina uhusiano mzuri na Tel Aviv na imekuwa ikiwakaribisha viongozi wa Israel kwa mikono miwili. Kwa msingi huo inatarajiwa kuwa Moscow itafanya mabadiliko ya kimsingi katika uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuchukua msimamo mpya kuhusu hatua za utawala huo katika masuala kama vile mienendo ya Tel Aviv kuhusiana na Wapalestina na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Syria.

Abdel Bari Atwan

Mchambuzi na mtaalamu wa Kiarabu, Abdel Bari Atwan anasema: "Hatutakuwa tumetia chumvi iwapo tutasema zaidi ya mara moja kwamba Israel itakuwa mshindwa na mhasirika mkuu katika mzozo wa Ukraine; kielelezo cha ukweli huu sio tu katika uhusiano wake na Russia, lakini pia kwa sababu mgogoro huu huenda ukawa mwanzo wa mwisho wa mamlaka na utawala wa Kimarekani iliouanzisha na kuukuza yenyewe."

Tags