UN: Idadi ya watu walio katika hatari ya njaa duniani inaongezeka
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa idadi ya watu walio katika hatari ya njaa duniani inaongezeka.
Kulingana na Shirika la Habari la Mehr, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kwamba idadi ya watu wanaosumbuliwa na njaa imefikia milioni 193.
FAO imesema katika ripoti yake ya kila mwaka kuwa watu wengine milioni 40 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa, ongezeko la watu walio katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa mwaka 2021 lilitokana na mkusanyiko wa mambo matatu ambayo ni mapigano, mgogoro wa hali ya hewa na majanga ya kiuchumi, ambavyo kwa pamoja vimeathiri watu katika nchi 53.
Nchi zilizoathiriwa zaidi ya tatizo hilo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Yemen na Afghanistan.
Katika upande mwingine wataalamu wameonya kuwa vita vya Ukraine vinaweza kuzidisha baa la njaa duniani.

Awali ripoti ya Hali ya Kibinadamu iliyochapishwa na UNICEF, ilisema shirika hilo linahitaji dola za Kimarekani milioni 351 ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 9.9 walioathiriwa na hali ya ukame katika maeneo manne ya Ethiopia.
Taarifa ya UNICEF pia imesema karibu watoto 650,000 wanaacha shule katika maeneo ya Oromia, Southern na Somali kutokana na hali ya ukame. Sambamba na hilo ilieleza kuwa hali ya ukame imelazimisha kufungwa kwa shule 2,000 kote nchini Ethiopia.