Russia: Mamluki wa Kizayuni wanapigana bega kwa bega na Waukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i83262-russia_mamluki_wa_kizayuni_wanapigana_bega_kwa_bega_na_waukraine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, mamluki wa Israel wanapigana bega kwa bega na vikosi vya jeshi la Ukraine
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
May 04, 2022 21:53 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, mamluki wa Israel wanapigana bega kwa bega na vikosi vya jeshi la Ukraine

Shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova alitangaza jana Jumatano kwamba mamluki wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanapigana pamoja na batalioni ya Azov inayoundwa na wanaharakati wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na ya kinazi nchini Ukraine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa unawaunga mkono Wanazi mamboleo nchini Ukraine.

Tuhuma za Zakharova zimekuja saa chache baada ya mashirika ya habari kuripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umekubali kupeleka msaada wa kijeshi kwa serikali ya Ukraine na kwamba maafisa wa Israel wanajadili suala la kuongeza misaada ya kijeshi kwa kyiv.

Ushahidi unathibitisha kwamba, Tel Aviv imefanya kile kinachoitwa chaguo la kihistoria na kuegemea upande wa Magharibi dhidi ya Russia, kwa kuzingatia matukio ya miezi ya hivi karibuni na kushadidi hatua za kambi ya Magharibi zinazoongozwa na Marekani dhidi ya Russia.

Wapiganaji Manazi wa Batalioni ya Azov, ukraine

Awali katika mahojiano yake na televisheni ya Italia, Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov alijibu swali kwamba, inakuwaje Moscow inadai kuwa inataka kuangamiza kabisa Unazi nchini Ukraine ilhali Rais wa nchi hiyo mwenyewe, Volodymyr Zelenskyy ni Myahudi? Sergei Lavrov amesema: "Hoja ya Zelenskyy ni kwamba 'Unazi unawezaje kuwepo Ukraine wakati yeye ni Myahudi?' Yumkini nikakosea, lakini ninavyoelewa mimi Adolph Hitler pia alikuwa na damu ya Kiyahudi."  

Uhusiano kati ya Russia na utawala wa Kizayuni wa Israel umeingia katika kipindi kipya na cha wasiwasi na mivutano baada ya kuanza mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine kutokana na misimamo ya Tel Aviv ya kuwa pamoja na nchi za Magharibi na kuchukua misimamo dhidi ya Russia.