Russia yasambaratisha ghala kubwa la silaha za Magharibi nchini Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i84676-russia_yasambaratisha_ghala_kubwa_la_silaha_za_magharibi_nchini_ukraine
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limesambaratisha ghala kubwa la silaha za nchi za Magharibi katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2022 22:45 UTC
  • Russia yasambaratisha ghala kubwa la silaha za Magharibi nchini Ukraine

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limesambaratisha ghala kubwa la silaha za nchi za Magharibi katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Russia wameteketeza ghala kubwa la silaha za Marekani na Ulaya katika mkoa wa Ternopil wa magharibi mwa Ukraine kwa kutumia makombora ya cruse.

Wizara hiyo ya Ulinzi ya Russia imesema pia kuwa, imeteketeza ndege tatu za kivita za Sukhoi Su-25 karibu na majimbo ya Donetsk na Kharkiv ya mashariki mwa Ukraine.

Tangu Russia ilipoanzisha operesheni maalumu ya kijeshi huko Ukraine tarehe 24 Februari 2022 hadi hivi sasa, wanajeshi wa Russia wameshateketeza ndege za kivitia 195, helikopta 130, droni yaani ndege zisizo na rubani 1,168 na vituo 336 vya kufyatulia makombora vya Ukraine. Aidha taarifa hiyo imesema kuwa, hadi hivi sasa jeshi la Russia limeshateketeza vifaru na magari mengine ya deraya 3,484 pamoja na magari maalumu ya kijeshi 3,538 ya Ukraine. 

Vita nchini Ukraine vimeisababishia hasara kubwa nchi hiyo

 

Mwanzoni kabisa mwa kuanzia vita vya Ukraine, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, lengo la vita hivyo ni kuyahami majimbo ya mashariki mwa Ukraine yaliyotangaza kujitenga na pia kupambana na magenge yenye fikra za kinazi ndani ya Ukraine na kuwapokonya silaha viongozi wa Kyiv ambao ni vibaraka wa Magharibi ambao nia yao hasa ni kurundika wanajeshi wa NATO katika mipaka ya Russia.

Vile vile viongozi wa Russia wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba, kitendo cha nchi za Magharibi cha kupeleka silaha zao Ukraine ni kuzidi kuiangamiza tu nchi hiyo, kwani vita vinapiganwa ndani ya ardhi ya Ukraine.