Harakati hatari za Marekani Mashariki mwa Asia
China imeitaka Marekani ikomeshe harakati zake hatari na za kichochezi eneo la Asia Mashariki ilikiwa ni pamoja na harakati zake za kijasusi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang Wenbin amesema Marekani inatumia zana za jeshi la anga na baharini kwa ajili ya kufanya ujasusi dhidi ya China na amesisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kulinda maslahi na usalama wa kitaifa wa nchi hiyo.
Miongoni mwa mambo yanayoashiriwa na China ni hatua ya Marekani ya kutumia ndege za kijasusi aina ya RC-135V dhidi ya nchi hiyo. Hata hivyo hapana shaka kuwa, serikali ya China inakusudia harakati pana zaidi za kijasusi za Marekani katika anga ya nchi hiyo, na tayari imeitahadharisha Washington kuhusiana na jambo hilo.
Tunaweza kuashiria kesi kadhaa kuhusiana na harakati hatari za Marekani kwa usalama wa kitaifa wa China. Kwanza kabisa ni kuendelea kuwepo kwa manuwari za kivita za Marekani katika maji ya kandokando ya China hususan katika lango bahari la Taiwan. Kuwepo kwa manuwari hizo kumeongeza tangu zama za utawala wa Donald Trump huko Marekani. Suala la pili ni vita vya mtandao (cyber war) kwa kadiri kwamba maafisa wa serikali ya China wanasema, mashambulizi mengi zaidi ya mtandaoni yaliyolenga mitandao ya nchi hiyo tangu mwaka 2018 yalifanywa na serikali ya Marekani.
Kane Ann ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mtandao wa China anasema: "Marekani sio tu kwamba ni mvumbuzi wa mtandao, bali pia inahusika na mashambulizi ya mtandaoni, na inayo teknolojia ya udukuzi."
Tatu ni vita vya kibiashara vya Marekani dhidi ya China. Japokuwa mivutano ya Washington na Beijing katika masuala ya kibiashara na kiuchumi imepungua kiasi ikilinganishwa na kipindi cha utawala wa Trump, lakini Marekani bado inaendeleza juhudi za kuizuia China kuingia katika masoko yake na kuwaimarisha washirika wake kwa ajili ya kuzima na kuzuia ushawishi wa Beijing katika masoko ya kimataifa.
Miongoni mwa mambo yanayoitia wasiwasi China kuhusiana na harakati hatari za Marekani ni njama ya Washington ya kutumia chakula kama wenzo wa mashinikizo dhidi ya Beijing. Suala hilo limeonekana zaidi baada ya mgogoro wa Ukraine ambapo tatizo la chakula limekuwa mgogoro wa kimataifa.
Mtaalamu wa masuala ya kimataifa Michael Kent anasema: "Japokuwa China ina wasiwasi kuhusiana na mambo hayo yote na inayapa uzito mkubwa, lakini jambo linaloitia wasiwasi mkubwa zaidi ni kadhia ya Taiwan na harakati kubwa za uharibifu za Marekani katika uwanja huu; na inaonakana kwamba China haiwezi kustahamili tena harakati hizi."
Alaa kulli hal, hatua ya Marekani ya kuendelea kuiuzia Taiwan silaha za kisasa ambayo imewatia jueri zaidi viongozi wa kisiwa hicho katika kukabiliana na China, na vilevile matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyeahidi kuilinda Taiwan mbele ya mashambulizi yoyote ya China, ni masuala muhimu ambayo New York Times inasema yamewatia viongozi wa Taiwan ujasiri wa kuzisukuma Marekani na China katika vita vya pande zote.