Kuchunguzwa uanachama wa Iran na upanuzi wa Jumuiya ya Shanghai
Kufuatia ufuatiliaji wa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO pamoja na kufanyika vikao vya mfululizo vya jumuiya hiyo katika ngazi mbalimbali, bila shaka jumuiya hiyo sasa inabadilika na kuwa muungano mkubwa katika bara kubwa la Asia na vilevile duniani.
Kwa mara nyingine suala la uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai limepangwa kujadiliwa katika vikao tofauti vya jumuiya hiyo ya kimataifa huko Uzbekistan. Kuhuu hilo Ghairat Fadhlov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uzbekistan ameashiria uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na kusema: Suala la uanachama wa Iran limepangwa kujadiliwa na kisha nyaraka kutiwa saini katika kikao cha viongozi ambacho kimepangwa kufanyika tarehe 15 hadi 16 za Septemba mwaka huu huko katika mji wa Samarkand.
Licha ya kuwa Iran ilichukua hatua za mwanzo za kupata uanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika kikao kilichofanyika mwezi Septemba mwaka uliopita, lakini ni wazi kuwa hatua za kukubaliwa uanachama wa nchi yoyote ile katika jumuiya hiyo kwa uchache zinapasa kuchukua miaka miwili. Washiriki wa kikao cha viongozi kilichofanyika mwaka uliopita huko Dushanbe, mji mkuu wa Tajikistan walitia saini kifurushi kikubwa cha nyaraka tofauti kuhusu suala hilo. Katika kipindi hicho pia vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa viliangazia pakubwa ukweli kwamba uamuzi uliochukuliwa na Baraza la Viongozi la nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO ndio ulikuwa uamuzi muhimu zaidi katika hatua za Iran kupewa uanachama katika jumuiya hiyo.
Kufuatia uanachama wa Iran, jumuiya ya SCO imekuwa ikiimarika siku baada ya nyingine na hasa ikitiliwa maanani kuwa uwepo wa Iran kwenye jumuiya hiyo umeinua nafasi na itibari ya jumuiya hiyo kimataifa na hivyo kuzifanya nchi nyingine kutaka kujiunga nayo. Nchi nyingi za kieneo na kimataifa tayari zimetoa maombi ya kutaka kujiunga nayo. Wachambuzi wa mambo wana mitazamo tofauti kuhusiana na umuhimu wa Iran kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
Kwa mfano Andre Sidirov, mkurugenzi mkuu wa Baraza la Masuala ya Kimataifa la Russia ambaye pia ni mtaalamu mashuhuri wa masuala ya kimataifa wa nchi hiyo anasema: Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai imebadilika kuwa jumuiya muhimu ya kimataifa mkabala wa kambi ya Magharibi kufuatia uanachama wa Iran na bila shaka inaweza kusimama imara mbele ya kiburi na mfumo wa kibeberu wa Magharibi inaoongozwa na Marekani.
Na hasa ikitiliwa maanani kwamba Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai imeasisiwa kwa msingi wa kukabiliana na mfumo wa uwepo wa kambi moja tu yenye nguvu duniani ambao inashajiishwa na kufuatiliwa na Marekani na bila shaka jumuiya hiyo itakuwa na nafasi kubwa katika kuanzisha mifumo mingine yenye nguvu katika pembe tofauti za dunia na hasa Iran, Russia, China na India. Kwa mtazamo huo, ni wazi kuwa iwapo falsafa ya kubuniwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni kuleta umoja katika bara kubwa la Asia basi inabainika wazi kuwa umoja huo hauwezi kukamilika bila kushirikishwa Iran. Na hasa kwa kutilia maanani kwamba kuwa na uhusiano na Iran ni suala linalofuatiliwa na kuchukuliwa na nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa suala lenye umuhimu wa kistratijia.
Bila shaka Iran na China zina maslahi mengi ya pamoja na wakati mwingine ya Kistrarijia katika eneo nyeti na muhimu la Ghuba ya Uajemi. Kwa mtazamo wa wajuzi wa mambo, Iran inaweza kuimarisha pakubwa nafasi ya China katika eneo la Bahari Hindi na Ghuba ya Uajemi. Mbali na hayo, Iran pia inaweza kuwa kizuizi cha kistratijia kwa manufaa ya China mbele ya tamaa ya Marekani kuhusiana na suala zima la Taiwan.