Iran yazitaka nchi za Shanghai kuwa jadi dhidi ya jinai za Israel na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani
(last modified 2024-10-17T02:54:06+00:00 )
Oct 17, 2024 02:54 UTC
  • Iran yazitaka nchi za Shanghai kuwa jadi dhidi ya jinai za Israel na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani

Mkuu wa ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mkutano wa Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai (SCO) huko Pakistan ameitaka jumuiya hiyo kuwa jadi na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya chokochoko za utawala wa Kizayuni na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani. Amezitaka nchi wanachama wa Shanghai kuchukua hatua za kivitendo ili kukabiliana na vikwazo vya kibiashara vya pande zote.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Muhammad Atabak Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza jana katika Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Pakistan kuwa Iran inataraji kuwa Jumuiya hiyo itakabiliana kwa sauti moja dhidi ya misimamo na hatua za upande mmoja na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani unaotekeleza dhidi ya raia wa nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Iran na kuzisaidia nchi wanachama wake ambazo zimeathiriwa na hatua hizo zilizo kinyume cha sheria kukabiliana na vikwazo vya Marekani. 

Nchi wanachama wa Jumuiya ya SCO 

Atabak amesema: 'Sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimelenga katika kuhakisha amani na usalama wa kanda hii hasa katika kupambana na ugaidi wa kitakfiri, vitendo vya uchupaji mipaka, magendo ya madawa ya kulevya na aina nyingine za jinai za kimataifa zilizoratibiwa.  

Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema suala la kupambana na vitendo vya uchupaji mipaka na ugaidi ambalo tangu awali liliwekwa katika ajenda ya kazi ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) linaendelea kutishia amani na usalama wa kanda hii. 

Amesema, Iran inaihesabu amani na uthabiti wa eneo kuwa ni uthabiti na utulivu wake yenyewe na hivyo haitaacha kufanya juhudi ili kudumisha uthabiti.  

Tags