Tabia ya dharau ya polisi wa Marekani dhidi ya wahamiaji
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanyika hivi karibuni, polisi wa kulinda usalama wa mipaka wa Marekani wamekuwa wakiamiliana na wahamiaji kwa njia ya dharau na kuwavunjia heshima.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa rasmi siku ya Ijumaa, maafisa wa polisi katika jimbo la Texas karibu na mpaka wa Marekani na Mexico wamekuwa wakichukua hatua zisizo za kitaalamu na za kuwavunjia heshima maelfu ya wahajiri wanaofika katika eneo hilo na ambao wengi ni raia wa Haiti waliojaribu kuvuka mpaka na kuingia Marekani mwezi Septemba 2021.
Hii ni katika hali ambayo muamala mbaya wa maafisa hao wa Marekani dhidi ya wahamiaji wa Haiti hivi karibuni uliamsha hasira kali ndani na nje ya Marekani.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa karibuni uliochapishwa na Umoja wa Mataifa, kivuko cha mpakani kati ya Mexico na Marekani ni kivuko hatari zaidi cha nchi kavu ulimwenguni.
Matokeo ya uchunguzi huo yametolewa wiki moja baada ya kupatikana miili 53 ya wahamiaji haramu ikiwa kwenye lori katika jimbo la Texas.
Tangu mwanzo wa mwaka huu hadi sasa wahamiaji haramu 493 ambao wamejaribu kuvuka mpaka wa Mexico kuingia Marekani wamepoteza maisha ikiwa ni ongezeko kubwa la wahanga ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.