China na Marekani zatunishiana misuli katika maji ya Visiwa vya Paracel
Jeshi la Wanamaji la China limeitimua manowari ya makombora ya Marekani ya USS Benfold iliyoingia bila kibali kwenye eneo la mpaka wa majini wa nchi hiyo katika Bahari ya China Kusini.
Katika miaka ya karibuni Marekani imeongeza harakati za kushadidisha mashinikizo dhidi ya China, ambapo mbali na kuchukua kadhaa za kichochezi ikiwemo ya kukiuzia silaha kisiwa cha Taiwan na kupiga doria katika eneo la majini la Bahari ya China Kusini, imekuwa ikitafuta kila fursa ya kuzitumia kwa maslahi yake tofauti na hitilafu zilizopo kati ya China na majirani zake katika eneo hilo la bahari ambao ni Vietnam, Taiwan, Malaysia, Brunei na Ufilipino.
Hivi karibuni, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilieleza katika ripoti kuwa inapinga ripoti iliyotolewa na China kuhusu mamlaka iliyonayo juu baadhi ya sehemu za Bahari ya China Kusini. Ripoti hiyo iliyotolewa na Beijing ilikuwa ya kwanza na aina yake katika miaka ya karibuni na imedhihirisha wasiwasi ilionao Washington juu ya nguvu na uwezo wa kijeshi wa China katika eneo la mashariki ya Asia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, jeshi la China limetangaza leo katika taarifa kwamba, limeifuatilia na kuitimua manowari moja ya makombora ya Marekani iliyoingia bila kibali kwenye Baharini ya China Kusini karibu na Visiwa vya Paracel.
Msemaji wa jeshi la China Tian Junli amesema, manowari moja ya makombora ya Marekani aina ya USS Benfold ilijipenyeza kinyume cha sheria na bila kuwa na kibali cha serikali ya China kwenye eneo la majini la China la Paracel.
Afisa huyo wa jeshi la China ametahadharisha kuwa, hatua kama hizo zinazochukuliwa na Marekani zina madhara makubwa kwa usalama na uthabiti wa Bahari ya China Kusini na zinakiuka sheria za kimataifa na taratibu za uhusiano wa kimataifa.../